• HABARI MPYA

    Friday, July 01, 2016

    YANGA SC YATAKA TFF IWAGHARIMIE USHIRIKI WAO KOMBE LA SHIRIKISHO

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Yanga, Yussuf Manji amesema kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linataka michezo ya klabu hiyo ya Kombe la SHirikisho Afrika, basi ichukue pia na gharama zote za maandalizi kabla ya kwenda kwenye michuano zikiwemo nauli, posho za wachezaji na kadhalika.
    Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo, Manji amesema kwamba watawapelekea TFF gharama hizo hivi karibuni na akamsihi Rais wa shirikisho, Jamal Malinzi asiigeuke kauli yake.
    "Maana sisi tumewaachia kutafuta fedha kwa ajili ya maandalizi ya mechi zinazokuja kulingana na uzito, tunaamini hatageuka,"amesema Manji katika taarifa yake. 
    Manji pia ameitaka TFF kutoingilia ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kama ilivyofanya mwaka jana, ilipoiruhusu Azam FC kufanya ziara ambayo ilikuwa nje ya ratiba na hivyo kufanya mabadiliko katika ratiba ya ligi hiyo.
    Mwenyekiti wa Yanga (kushoto), Yussuf Manji akiwa na Makamu wake, Clement Sanga
    Amesema TFF ilipaswa kutoa mjumbe wa masuala ya kisheria kutoka TFF kwenda na Yanga Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho kuwania hatua ya makundi dhidi ya wenyeji Sagrada Esperanca, ambako timu yao ilifanyiwa fujo na kupigwa na polisi wa nchi hiyo. "Matokeo yake, badala ya kutuunga mkono katika kupeleka rasmi malalamiko yetu kwenda Shirikio la Soka la Afrika (CAF), TFF lilikaa kimya. Ilibidi itupe vifaa vya CAF vilivyotumwa kwa ajili ya kutumika katika hatua za makundi kwa wakati unaotakiwa, jambo ambalo halikufanyika na kutufanya tuingie gharama ambazo hazikuhitajika na kutusababishia adhabu kutoka CAF,".
    "Ilibidi ichukue hatua kutokana na kuonyeshwa kwa klabu yetu kadi nyingi mno za njano (8) na kadi moja nyekundu katika mchezo wa kundi letu nchini Algeria dhidi ya klabu ya MOB,".
    "Ingehakikisha  inatuonyesha wazi tarehe na muda wa mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ambapo badala yake waratibu waliamua kuupanga mchezo huo dhidi ya TP Mazembe dhidi ya maslahi ya Yanga.  Hali hiyo ilizidi kuvurugwa kwa kufikiwa mkataba wa siri na Azam TV wa kuurusha nchini Tanzania mchezo huo wa Yanga wakati klabu ilikuwa imepiga hatua katika majadiliano  ya shirika la utangazaji ya TBC (ambao mwaka jana walikuwa wamepokea magari matatu kutoka China ili kuimarisha matangazo ya moja kwa moja ambayo yaligharimu kiasi cha Shilingi bilioni 5 kwa kila gari) kwa ajili ya kwa ajili ya kiwango kinachotakiwa katika kurusha matangazo kimataifa,".
    "Pia ilibidi kuipa Yanga fedha za CAF kwa kufuzu kuingia katika hatua hiyo ya mashindano ambayo ilifahamika kuwa ni Dola 15,000 za Marekani;  fedha za Kombe la FA katika mchezo wake na Azam FC; Zawadi ya VODACOM ya Ligi Kuu, zote hizo zikisemekana kuwa ni kiasi cha Sh. Milioni 500, ambazo iwapo zingelipwa na TFF katika muda mwafaka, Yanga ingezitumia fedha hizo kukabiliana na majukumu mbalimbali ya fedha ikiwa ni pamoja na bonasi za wachezaji hadi usajili wa wachezaji katika dirisha maalum la CAF, na kadhalika,".
    "Mahali ambapo klabu inasimama leo hii ni kutokana na juhudi zake yenyewe na si kutokana na ushirikiano au msaada wowote ambao Yanga imeupata kutoka  TFF ambapo Yanga kamwe haikuutegemea na ambapo imeona waziwazi kwamba TFF imeshindwa kuisaidia,".
    "Uamuzi wa Yanga kuwaruhusu mashabiki wa soka kuingia bure katika mchezo huo ili kuweza kumpata mchezaji “halisi japokuwa wa kufikirika” wa 12 si jambo jipya katika soka, japokuwa jambo hilo limekwenda kinyume na matakwa ya TFF ambayo ilitegemea kufanya makato mbalimbali ambayo  yamefutwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA),".  
    "Pamoja na hayo yote, kama TFF wanataka kusimamia michezo yetu, basi wachukue gharama zote za maandalizi kabla ya kwenda kwenye michuano kama nauli, posho za wachezaji na kadhalika, hesabu tutawapelekea hivi karibuni. Tunammsihi Rais wa TFF asigeuke kauli yake maana sisi tumewaachia kutafuta fedha kwa ajili ya maandalizi ya mechi zinazokuja kulingana na uzito, tunaamini hatageuka,". 
    "Tunashangaa CAF na TFF walikuwa wapi wakati rais mstaafu Jakaya Kikwete katika mchezo wake wa kwanza katika  Uwanja wa Taifa alipowaruhusu mashabiki kuingia bure?  Inabidi wafahamu pia kwamba tulipocheza huko Angola na Algeria, mashabiki waliruhusiwa kuingia viwanjani bure tulipocheza huko.  Sisi kama klabu tunawathamini mashabiki wetu katika kututia hamasa wakati tunacheza,". 
    "Mimi mwenyewe nilitoa fursa hiyo huko Mwanza miaka ipatayo kumi iliyopita wakati klabu ilicheza dhidi ya El-Merreikh, na hapakuwepo na adhabu yoyote kutoka CAF kutokana na hatua hiyo.  Je, TFF wanatufanyia hivi kama kutuadhibu kutokana na kukosa mapato ambayo yangeliwezesha kufanikisha sikukuu ya Idd el Fitri?,"
    "Uamuzi wa kuwaruhusu mashabiki kuingia bure Uwanja wa Taifa ni jambo lenye busara nyepesi kufahamika kwa mtu yeyote.  Katika mchezo huo ambao ulipigwa uwanjani hapo, mapato yasingezidi Sh. 100 Milioni, na baada ya makato yote ambayo yangehitajika kufanyika, klabu ingejikuta imebaki na kiasi cha Sh. 40 Milioni.  Hii ni kwa kuchukulia kwamba pasingefanyika wizi wowote kwenye milango na pasingekuwepo na tiketi bandia, hali ambayo hufanywa katika michezo ambayo husimamiwa na TFF hasa ile ya ligi,".
    "Binafsi niliamua kwamba kwa vile Uwanja wa Taifa ulikuwa umekodishwa kwa ajili ya maonyesho ya starehe kwa Sh. 20 Milioni ambapo kwa uelewa wangu  kiasi hicho kilikuwa kimefutwa na Waziri wa Michezo na Utamaduni kwa kuwa Yanga ilikuwa inawakilisha taifa. Klabu iliona ingebeba gharama zingine mbalimbali zenye kuhusika na mchezo huo, yote hayo kwa ajili ya kutaka mashabiki wengi wa Tanzania waingie ili kuitia moyo Yanga katika siku hiyo ya mchezo,".
    "Niliongea na vyombo vya usalama, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu nia hiyo ya Yanga, ambapo  jeshi la polisi lilifanya kazi nzuri sana. Hali ya uwanjani ilikuwa tulivu kabisa isipokuwa nje ambako baadhi ya mashabiki waliuziwa tiketi feki ambazo tunahisi zilikuwa zimetayarishwa na TFF. Hata hivyo, polisi waliweza kudhibiti hali hiyo ambapo hakuna aliyejeruhiwa au kukamatwa, jambo ambalo linaonyesha wazi kwamba woga wa CAF wa kuiadhibu Yanga kutokana na kinachodaiwa vurugu, ni upuuzi mtupu,".
    "Kuhusu suala la kutakiwa mashabiki  40,000 pekee waingie katika uwanja huo wenye kubeba watu  60,000, jambo ambalo lilizua sababu kutoka CAF kuiadhibu kwa kuipiga faini Yanga, ninashangaa ni busara gani ilitumiwa na serikali katika kujenga uwanja wa kuingiza watu 60,000 na badala yake kutegemea uingize watu 40,000 tu!  Rais wa TFF hakupewa habari za kweli. Ninachofahamu ni kwamba mratibu wa mechi alisema kwamba maofisa wa TFF walitaka waingie watu 40,000 tu ili kuipunguza nguvu Yanga lakini alikataa, kwani hakuona sababu ya watu kuingia na kuujaza uwanja kama ilivyo kawaida,".
    "Isitoshe,  Kamishna huyo ninaweza kumleta mbele ya Watanzania wasikie jinsi TFF ilivyokuwa inajaribu kumpotosha dhidi ya Yanga kwa vile klabu hiyo ilikuwa imeamua kuionyesha mechi hiyo bure na kuvinyima fursa vituo fulani vya televisheni  kuuonyesha mchezo huo, pamoja na kuvuruga mipango ya TFF ya kupata fedha kutokana na mauzo ya tiketi.  Katika hili, nina fahari kubwa kwa kutoa fursa kwa zaidi ya mashabiki 60,000 kuiona mechi hiyo bure ambayo hata kama hatukushinda lakini tulikuwa pamoja kama Watanzania,".
    "Nawajulisha wananchi kwamba uhasama kati ya TFF na Yanga si mpya kwani hata katika uchaguzi tuliofanya majuzi, kulikuwa na majaribio ya kutaka kuvuruga matokeo yake, na njama hizi zimefikishwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).  
    Ni vyema TFF ikashughulikia matatizo yake mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kupanga matokeo ya mechi mbalimbali, kuingilia masuala ya klabu mbalimbali kama ilivyofanywa kwa Yanga kwa kujaribu kutumia katiba ya zamani ya mwaka 2010, kuingia mikataba ya siri na wadhamini wa ligi, haki za vituo vya televisheni kuonyesha mechi na kusababisha kuziua klabu kifedha, na  kujifanya kuchukua hatua za maendeleo katika soka kwa unafiki wa kutegemea kodi mbalimbali kutoka Yanga na Simba. Sisi katika klabu ya Yanga tuliokuwa katika Kamati ya Utendaji hatuchukui hata posho za vikao kwani tunataka kwanza kuifanya klabu ijitegemee kifedha kabla ya maslahi yetu binafsi.  Kinyume chake, posho ndani ya TFF limekuwa jambo la kawaida, hali ambayo imefanya hata mahesabu yake yasichapishwe kwa ajili ya kupitiwa waziwazi na kila mtu,".
    "Nasisitiza kwamba katika uchaguzi uliofanyika majuzi, kabla ya hapo nilikuwa Mwenyekiti nikiwa nimechaguliwa kwa kura kwa kipindi cha miaka miwili katika uchaguzi mdogo nikiwa nimeapa kuleta uaminiano kati ya mashabiki na viongozi wa klabu, ambapo kipindi hicho kiliongezwa baadaye kwa mwaka mmoja na wanachama wa klabu, na kuongezwa tena kwa mwaka mmoja kutokana na kufanyika uchaguzi mkuu mwaka jana kutokana na ushauri wa maandishi wa TFF,".
    "Nimesema wazi kufuatia uchaguzi wa majuzi kwamba nitapigania maendeleo  ya klabu kwani hapatakuwa na  cha kufurahia na kuleta amani na utulivu katika klabu iwapo Yanga itashindwa kushiriki katika michuano ya soka barani Afrika, jambo ambalo mashabiki wa Yanga wanalitaka siku zote,".
    "Pia ninanyoosha mkono wa urafiki kwa klabu ya Simba kwa uchaguzi wao, japokuwa wao hawakufanya hivyo niliposhinda.  Nimeelekeza kwamba utani (ushindani) kati ya Simba na Yanga uwe katika viwanja vya soka, ndiyo maana katika mechi yetu na TP Mazembe niliwakaribisha kama Watanzania wenzetu, tuliwaheshimu wote  pamoja na wale waliovaa majezi na kuishangilia TP Mazembe,".
    "Mkono huo wa kutakiana mema sitaki ubadilike na kuwa ngumi, bali uendeleze ushirikiano, na TFF iache njama zake dhidi ya Yanga bali iungane nasi katika kujenga soka la Tanzania,".
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YATAKA TFF IWAGHARIMIE USHIRIKI WAO KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top