• HABARI MPYA

  Wednesday, July 13, 2016

  TUSIDANGANYANE, HATUKO TAYARI KWA SOKA LA UFUKWENI KIMATAIFA

  TANZANIA itacheza na Ivory Coast kuwania kufuzu Fainali za Soka ya Ufukweni nchini Nigeria baadaye mwaka huu.
  Mechi ya kwanza imepangwa kufanyika mjini Abidjan nchini Ivory Coast kati ya Agosti 26, 27 na wakati marudiano yatafanyika mjini Dar es Salaam kati ya Septemba 16, 17 na 18, mwaka huu.
  Timu nyingine zilizomo kwenye kinyang’anyiro hicho mbali ya Tanzania na Ivory Coast ni Cape Verde, Ghana, Misri, Liberia, Libya, Kenya, Madagascar, Morocco, Msumbiji, Senegal, Sudan na Uganda.
  Kutakuwa ne mechi moja moja tu za kuwania kufuzu ambapo washindi saba wataungana na wenyeji Nigeria kwenye fainali hizo zinazotarajiwa kuanza Desemba 13 hadi 18, mwaka huu.
  Timu zitakazoingia fainali ya michuano hiyo, zitaiwakilsha Afrika kwenye Kombe la Dunia la FIFA la Soka ya Ufukweni ambalo fainali zake zitafanyika Bahamas kuanzia Aprili 27 hadi Mei 7 mwaka 2017. 
  Ikumbukwe Madagascar ndiyo walikuwa mabingwa wa mwaka 2015 baada ya kuifunga Senegal kwa penalti 2-1 kwenye fainali nchini Shelisheli.
  Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilishiriki michuano ya soka la ufukweni mwaka jana kutolewa ‘kwa aibu’ na Misri ikifungwa nyumbani na ugenini.
  Na wakati ratiba ya mechi za kufuzu Fainali za soka la Ufukweni inatoka, mwaka huu Tanzania hakujafanyika mashindano yoyote ya mchezo huo, tofauti na mwaka jana kulifanyika mashindano maalum ya kutafuta wachezaji wa kuunda timu hiyo.  
  Mechi na Ivory itachezwa Agoti na hadi sasa katikati ya Julai hakuna mashindano yaliyofanyika wala dalili za kufanyika – maana yake ni vigumu kupata wachezaji bora wa kuunda timu ya taifa ya soka la ufukweni.
  Lakini kwa ujumla Tanzania haijaingia rasmi kwa vitendo kwenye soka la ufukweni na hakuna mashindano rasmi ya mchezo huo.
  Hapo ndipo ninapojiuliza tunawezaje kuingia katika soka ya ufukweni kimataifa wakati hapa nyumbani hatujawa na soka ya ufukweni rasmi?
  Na kwa kuwa hatukuwa na mashindano ya Soka la Ufukweni tangu tulipotolewa na Misri mwaka jana, je timu itakayoundwa itatokana na wachezaji gani?
  Kwa dalili zote, bado hatujawa tayari kwa soka ya ufukweni kimataifa, zaidi ya kuanza kuujenga mchezo huo nyumbani kwanza kama tunataka kuucheza kimataifa.
  Wazi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutenga bajeti kwa ajili ya Soka la Ufukweni ni ufujaji wa fedha ambazo zingesaidia maandalizi ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys au timu ya wanawake, Twiga Stars, ambazo hazina wadhamini.    
  Ukweli ni kwamba TFF wanapaswa kujitoa tu kwenye soka la ufukweni kimataifa na kuanza kujijenga kwanza hapa nyumbani kwa kuhakikisha kwanza kunakuwa na mashindano yatakayosaidia kuzalisha wachezaji bora, ambao ndiyo watakuja kuunda timu ya taifa, hatimaye kurejea kwenye soka ya kimataifa tukiwa tayari.
  Lakini kutaka kulazimisha kucheza hivi sasa ni ubabaishaji na kupoteza fedha ambazo zitatumika kuigharamia timu hiyo kushiriki mashindano hayo, ambazo pengine zingezisaidia Serengeti Boys na Twiga Stars. 
  Mwaka huu TFF imeshindwa kuiingiza timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kwenye mechi za kufuzu Fainali za Afrika kwa madai hawaamini kama wana U-20 iliyo tayari.
  Na Rais wa TFF, Jamal Malinzi akasema kwamba wameingiza U-17 pekee wakiamini hiyo ndiyo itakuwa U-20 halisi miaka miwili ijayo na hapo watarudi kwenye kwenye mashindano hayo.
  Kila timu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inapaswa kuwa na timu ya vijana ya U-20 kwa mujibu wa kanuni – lakini TFF imeona haiwezi kushiriki mechi za kufuzu Fainali za U-20 Afrika kwa sababu haiamini kama ina timu iliyo tayari.
  Tuna timu za U-20 zipatazo 16 kutoka timu za Ligi Kuu, lakini tumekosa vijana 20 wa kuunda timu ya taifa – je, katika Soka la Ufukweni ambako hakuna mashindano na maana yake hakuna timu, tutapataje timu ya taifa?
  Mambo mengine hayahitaji ushauri wa wataalamu kutoka nje – ni kiasi cha kujifikiria tu na kuangalia hali halisi kisha kufanya maamuzi sahihi.
  Ukweli ni kwamba hatuko tayari kwa mashindano ya kimataifa ya soka ya Ufukweni. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUSIDANGANYANE, HATUKO TAYARI KWA SOKA LA UFUKWENI KIMATAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top