• HABARI MPYA

    Wednesday, July 06, 2016

    OMOG ATAKIEPUKAJE KIKOMBE HIKI SIMBA SC?

    UKIFUATILIA vyombo vya Habari England kwa sasa utakuta vimeanza kubashiri mifumo ambayo Manchester United na Manchester City zitaanza kutumia msimu ujao.
    Vimeza kutabiri aina ya soka ambayo timu hizo zitakuwa zinacheza na aina ya wachezaji ambao hawatakuwa na nafasi tena katika timu hizo.
    Hiyo ni kutokana kuwafahamu vyema makocha wapya wa timu hizo, Mreno Jose Mourinho wa United na Mspanyola Pep Guardiola wa Man City.
    Mourinho amewahi kufundisha kwa awamu mbili Chelsea ya England, lakini Guardiola pamoja na kwamba anakwenda kwa mara ya kwanza nchini humo, lakini kazi yake inafahamika vyema kutokana na mafanikio yake Barcelona ya kwao na Bayern Munich ya Ujerumani.
    Hivyo ndivyo huwa, timu za wenzetu huchukua makocha kulingana na falsafa zao wakizioanisha na falsafa za klabu zao.
    Kwa hapa Tanzania falsafa maarufu ya Simba SC ni soka ya pasi nyingi na burudani, wakati mahasimu wao ni soka ya pasi ndefu, kasi na nguvu.
    Miaka ya nyuma falsafa hizo zilienziwa vizuri kwa kuanzia kutazama aina ya kocha ambaye anachukuliwa na hata wachezaji wanaosajiliwa.
    Lakini mambo haya taratibu huku kwetu yanaanza kupotea na sasa timu zinaajiri makocha kwa sababu ya wasifu wao na hawazingatii kama falsafa yake itaendana na ya klabu.
    Na hata katika kusajili imekuwa hivyo hivyo – wanatazama mchezaji mzuri tu bila kumfikiria kama atafiti katika falsafa ya klabu.
    Na ndiyo maana sasa utaona Yanga wamebadilika wanapiga pasi nyingi na  na Simba SC ndiyo ndiyo wamegeuka kucheza soka ya mipira mirefu.
    Lakini makocha wanapobadilika na aina ya soka hubadilika pia – kwa sababu viongozi wanaajiri makocha bila kuzingatia falsafa ya asili ya klabu.
    Lakini kitu kibaya zaidi ni kwamba wanasajiliwa wachezaji kwanza, ndiyo mwalimu anafuatia.
    Wiki iliyopita Simba SC iliingia Mkataba wa miaka miwili na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kuifundisha klabu hiyo – ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Muingereza, Dylan Kerr aliyeondolewa Januari mwaka huu.
    Kwa kusaini Mkataba huo, Simba inakuwa klabu ya pili kwa Omog kufundisha Tanzania baada ya awali kuwa na Azam FC, aliyoiongoza kwa msimu mmoja na nusu ikishinda mechi 30 kati ya 55 za mashindano yote, sare 14 na kufungwa 11.
    Omog ni kocha mkubwa, mwenye rekodi nzuri na aliyefanya kazi katika nchi zaidi ya kwa mafanikio – maana yake Simba imeajiri kocha mzuri.
    Omog aliyeipa Leopard FC ya Kongo Brazaville Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2014, enzi zake alichezea Yaounde na ni mwalimu wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na mazoezi ya viungo aliyehitimu vizuri mafunzo yake katika Chuo cha Vijana na Michezo, INJS mjini Yaounde, Cameroon. 
    Alikwenda kujiendeleza kielimu nchini Ujerumani na kwa pamoja na Pierre Njili na Martin Ndtoungou walipata Stashahada za ukocha na leseni za UEFA daraja la B mwaka 1987 na aliporejea alifundisha timu kadhaa kama Fovu ya Baham na Aigle ya Menoua na akazifikisha fainali ya Kombe la Cameroon klabu zote. 
    Mwaka 2001 aliteuliwa kuwa Msaidizi wa kocha Mjerumani, Winfried Schafer katika timu ya taifa ya Cameroon, Simba Wasiofungika chini ya Nahodha Samuel Eto’o haswa kutokana na kujua kwake Kijerumani, kwa sababu kocha huyo alikuwa hazungumzi Kiingereza wala Kifaransa, lugha zinazotumika nchini humo. 
    Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa kocha Mkuu wa timu ya taifa baada ya kuondoka Winfried Schafer, lakini akafukuzwa mwaka 2010 kutokana na kushindwa kuiwezesha Cameroon kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika. Akaamua kutoka nje ya nchi na mwaka 2011 alijiunga na AC Leopard ya Kongo, ambayo aliiwezesha kutwaa Kombe mwaka huo huo na kuipa tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho. 
    Na akafanikiwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe hilo la Afrika mwaka 2012 kwa kuifunga Djoliba ya Mali mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano na kutengeneza ushindi wa jumla wa 4-3. Mwaka 2014 alijiunga na Azam FC ambayo aliipa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu.  
    Lakini pamoja na wasifu huu mzuri ambao unamaanisha Simba imepata kocha bora, lakini tayari kuna wasiwasi kama atadumu.
    Ameingia katika timu ambayo ipo mbioni kukamilisha usajili wake – ina maana atakuta wachezaji ambao si chaguo lake aanze kuwandaa kulingana na falsafa zake.
    Manchester United walipojua tu watakuwa na kocha mpya, Mourinho basi walihakikisha wanamalizana naye mapema ili aanze kusajili.
    Lakini Simba tangu Januari baada ya kumfukuza Kerr ilijua italeta kocha mpya, ila ilishindwa kupanga vyema ratiba zake, ili mwalimu mpya awahi kusajili.
    Kwa vyovyote, Omog atakuwa na msimu mgumu wa kwanza Simba SC na wazi atahitaji muda ili kuanzia msimu ujao aanze kuunda timu yake.
    Lakini hakuna hakika kama iwapo timu haitakuwa na matokeo mazuri atavumiliwa. Simba wanawatoa kafara makocha ili kujisafisha kwa wapenzi na wanachama, lakini hawajui kwamba ndiyo wanajiharibia zaidi.
    Kwa sababu kwa kufukuza makocha ovyo, timu imekuwa ikianza upya kila msimu na matoeko yake sasa wanakwenda msimu wa nne bila kutwaa taji wala kushika japo nafasi ya pili katika Ligi Kuu.
    Simba hawana woga tena wa kufukuza kocha – na ndiyo hapo ninapojiuliza Omog atakuwa na bahati gani akiepuke kikombe hicho?        
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OMOG ATAKIEPUKAJE KIKOMBE HIKI SIMBA SC? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top