• HABARI MPYA

  Monday, July 18, 2016

  NI AIBU KUSHANGILIA TIMU ZA NJE – NCHEMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mwigullu Nchemba amesema ni aibu kwa mashabiki wa soka nchini kushangilia timu za nje na akashauri desturi hiyo iachwe mara moja.
  Akizungumza usiku wa jana katika hafla ya utoaji wa tuzo za washindi mbalimbali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Waziri Nchemba alisema ni vyema Watanzania wakaonyesha uzalendo kwa timu zao.
  “Inakuja timu ya nje, mtu anabeba bendera ya nje anaishangilia, anaacha kushangilia bendera ya nyumbani, hii si picha nzuri,”alisema Nchemba ambaye inafahamika ni mpenzi wa Yanga.
  Waziri huyo akatolea mfano wa Nahodha wa timu ya taifa, Mbwana Samatta kwamba alionyesha uzalendo kwa nchi yake kwa kubeba bendera ya Tanzania baada ya kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika Januari mwaka huu. 
  Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akizungumza jana katika hafla ya utoaji tuzo za washindi wa Ligi Kuu
  Samatta alishinda tuzo hiyo baada ya kuipa TP Mazembe ubingwa wa Afrika na kuibuka mfungaji bora – lakini baada ya mafanikio hayo akanunuliwa na KRC Genk ya Ubelgiji.
  Aidha, Waziri Nchemba alisema kwamba Serikali bado iko macho na suala la upangaji matokeo, rushwa na matumizi ya dawa zisizoruhusiwa mchezoni.
  Alisema kwamba michezo nchini haiwezi kufanikiwa kama vitendo hivyo haramu vitaendelea kufumbiwa macho.
  "Wizara yangu kwa kushirikiana na ile ya Michezo pamoja na utumishi wa umma tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha tunakomesha tabia hizo.
  Lazima tufahamu kuwa vitendo kama hivi tukiacha viendelee kufanyika soka letu halitopiga hatua," alisema Mwigulu
  Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alisema wataendelea kupambana na vitendo vya rushwa na upangaji matokeo.
  Waziri Nchemba (kushoto) na Rais wa TFF, Jamal Malinzi wakifurahia jambo jana

  “Mtu yeyote atakayediriki kupanga matokeo nitakufa naye. Suala hili nitahakikisha nalikomesha kwenye utawala wangu. Sitamuangalia mtu usoni, kwa sababu madhara yake ni makubwa,”alisema.
  Na kuhusu tatizo la ubadilishwaji holela wa ratiba za mashindano, hususan Ligi Kuu, alisema hilo linasababishwa Jiografia ya nchi. 
  “Mazingira yetu siyo rafiki kuweza kupanga ratiba ambayo itazipa nafasi timu zetu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa. Tutajitahidi ratiba iwe nzuri, ila kiukweli ni suala ambalo haliepukiki,”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI AIBU KUSHANGILIA TIMU ZA NJE – NCHEMBA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top