• HABARI MPYA

    Thursday, July 21, 2016

    MFARANSA ALIYETUPIWA VIRAGO OMAN AWA KOCHA MPYA NIGERIA

    SHIRIKISHO la Soka Nigeria limemteua kocha aliyefukuzwa Oman, Mfaransa Paul Le Guen kuiongoza timu hiyo katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018, ambako wamepangwa kundi gumu na Algeria, Cameroon na Zambia.
    Kocha wa zamani wa Cameroon, Le Guen amewapiku Mbelgiji Tom Sainfiet na Salisu Yusuf, ambaye alikuwa kocha wa muda wa Super Eagles tangu Mei.
    "Paul Le Guen ameteuliwa kuwa kocha mpya wa Nigeria na atasaidiwa na Yusuf na Imma Amakapabo wa Enugu Rangers," amesema Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Paul Bassey.
    Aliiongoza Cameroon katika Kombe la Dunia mwaka 2010 na amefundisha klabu kubwa Ufaransa, zikiwemo Lyon na Paris Saint Germain, pamoja na za Rangers ya Scotland.
    Mfaransa Paul Le Guen ameteuliwa kuiongoza Nigeria katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018 

    Mara ya mwisho alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Oman, ambako alifukuzwa Novemba mwaka 2015 baada ya kuanza vibaya mechi za kufuzu Kombe la Dunia.
    Le Guen mwenye umri wa miaka 52, ametambulishwa kama Mshauri wa Ufundi na Yusuf mmoja wa Wasaidizi wa Kocha na atakuwa akilipwa dola za Kimarekani 50,000 kwa mwezi, ambazo zitakuwa zinalipwa na kampuni binafasi baada ya Serikali kujitoa.
    Jukumu la kwanza la Le Guen, aliyeipa Lyon mataji matatu ya Ligue 1 kati ya mwaka 2002 na 2005, ni kuisaidia Super Eagles kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya sita, akianza na safari ya Zambia Oktoba.
    Na anaichukua timu hiyo ikiwa tayari imepoteza nafasi ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya pili mfululizo na sasa mabingwa hao mara tatu wa Afrika wanashika nafasi ya 70 katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MFARANSA ALIYETUPIWA VIRAGO OMAN AWA KOCHA MPYA NIGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top