• HABARI MPYA

    Tuesday, January 20, 2026

    HATIMAYE MWAMBA WA LUSAKA CHAMA AREJEA SIMBA SC


    KIUNGO Mzambia, Clatous Chota Chama (34) amerejea klabu ya Simba SC kwa mara ya pili baada ya msimu mmoja na nusu tangu aondoke mara ya mwisho.
    Simba SC imemtambulisha rasmi Mwamba wa Lusaka kurejea kikosini akitolea Singida Black Stars ambako amedumu kwa nusu msimu kufuatia kuwasili akitokea kwa vigogo wengine nchini, Yanga SC.
    Chama anayejulikana kwa jina la utani la Triple C’ aliwasili Tanzania kwa mara ya kwanza Julai mwaka 2018 kujiunga na Simba SC akitokea Lusaka Dynamos FC ya kwao, Zambia.
    Agosti mwaka 2021 Simba ilimuuza Chama RSB Berkane ya Morocco, ambako hata hivyo mambo hayakumuendea vizuri akarejea Msimbazi  baada ya nusu msimu, Januari mwaka 2022.
    Nyota ya Chama ikaendelea kung’ara Msimbazi akicheza kwa misimu miwili kabla ya kuhamia kwa watani wa jadi, Yanga Julai 2024 ambako alicheza kwa msimu mmoja kabla ya kuhamia Singida Black Stars.
    Chama ni mchezaji aliyeibukia klabu maarufu, Nchanga Rangers FC mwaka 2010, kabla ya kuhamia ZESCO United FC mwaka 2013 zote za Zambia. 
    Januari mwaka 2017 alivuka mipaka ya Zambia kwa mara ya kwanza alipokwenda kujiunga na Ittihad Alex ya Misri, ambako baada ya mwezi mmoja na ushei akarejea nyumbani kujiunga na Lusaka Dynamos FC.
    Anakuwa mchezaji mpya wa tano mpya kwa Simba SC dirisha hili dogo baada ya kipa Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo (29) kutoka AS FAN Niamey ya kwao, Niger na beki wa kushoto mzawa, Nickson Clement Kibabage (25) kutoka Singida Black Stars ya nyumbani,
    Wengine ni beki wa kati, Ismaël Olivier Touré (28) kutoka FC Baniyas ya Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na winga wa kushoto Msenegal, Libasse Gueye (22) kutoka Teungueth FC ya kwao.
    Next
    This is the most recent post.
    Older Post
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATIMAYE MWAMBA WA LUSAKA CHAMA AREJEA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top