• HABARI MPYA

  Wednesday, July 13, 2016

  TAMBWE AREJESHA MATUMAINI YA KUIVAA MEDEAMA, AJIFUA ‘MDOGO MDOGO’ LEO

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe leo ameweza kufanya mazoezi mepesi baada ya kupata nafuu ya ugongwa wa Malaria.
  Tambwe alishindwa kabisa kufanya mazoezi kwa siku tano zilizopita kutokana na kusumbuliwa na Malaria, lakini leo aliibuka Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam na kufanya mazoezi mepesi.
  Kama ataendelea na siku mbili zijazo kufanya mazoezi, maana yake Tambwe anaweza kurudishwa kwenye programu za mchezo wa Jumamosi dhidi ya Medeama FC ya Ghana.
  Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, aliyelazimika kuwekewa dripu sita mwishoni mwa wiki ili kurejesha nguvu mwilini mwake, leo alifanya mazoezi chini ya uangalizi wa Daktari.
  Amissi Tambwe akifanya mazoezi mepesi leo Uwanja wa Boko Veterani
  Yanga inatarajiwa kumenyana na Medeama FC ya Ghana katika mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm anamuhitaji Tambwe kwa ajili ya mchezo huo.
  Tambwe aliukosa mchezo uliopita dhidi ya TP Mazembe kutokana na kuwa anatumikia adhabu ya kadi – na sasa anapambana na Malaria ili acheze Jumamosi.
  Yanga inaendelea na mazoezi Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam huku ikiwa imeweka kambi hoteli Ludger Plazza, Kunduchi kujiandaa na mchezo wa tatu wa kundi lake.
  Tayari Yanga SC itawakosa beki Mwinyi Hajji Mngwali, viungo Deus Kaseke na Geoffrey Mwashiuya katika mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.
  Kaseke aliumia kwenye ajali ya pili, wakati Mngwali na Mwashiuya wote wanasumbuliwa na maumivu ya goti na hawataweza kucheza mchezo huo Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga inahitaji ushindi dhidi ya Medeama baada ya kupoteza mechi zote mbili za mwanzo wakifungwa 1-0 mara zote – na Mo Bejaia nchini Algeria Juni 19 na TP Mazembe ya DRC Dar es Salaam Juni 28.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAMBWE AREJESHA MATUMAINI YA KUIVAA MEDEAMA, AJIFUA ‘MDOGO MDOGO’ LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top