• HABARI MPYA

    Monday, May 07, 2018

    TFF YAAGIZA YANGA KUFANYA UCHAGUZI HARAKA, MKWASA ATAJA SABABU ZA KUTOVAA JEZI ZA WADHAMINI JANA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Yanga ya Dar es Salaam kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi wake waliojiuzulu, ikiwemo ya Mwenyekiti.
    Kwa mujibu wa barua ya Kaimu, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Herman Julius kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho hilo, Revocatus Kuuli pamoja na Yanga SC, klabu nyingine zinazotakiwa kufanya uchaguzi ni AFC ya Arusha na Coastal Union ya Tanga.
    “Klabu za mpira wa miguu zinatarajiwa kufanya uchaguzi wa viongozi wapya/kuziba nafasi zilizo wazi katika safu za uongozi wao hivi karibuni,”imesema barua hiyo iliyozitaja AFC, Yanga na Coastal.
    Ikumbukwe Yanga imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji Mei mwaka jana.
    Wanachama wa Yanga wanatakiwa kujipanga kuchagua viongozi wapya
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.

    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Hali hiyo ilisababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ya kiufadhili Yanga na kufanya wachezaji wakose mishahara kwa kipindi chote hicho kabla ya viongozi wenzake kuanza kufanya jitihada za kulipa taratibu.
    Kwa sasa hali ni ngumu mno ndani ya klabu ya Yanga pamoja na kuwepo kwa wadhamini, kampuni za SportPesa, Macron, Azam TV na maji ya Afya.
    Wakati huo huo: Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema timu haikuvaa jezi zenye nembo ya wadhamini, kampuni ya SportPesa jana wakifungwa 4-0 na USM Alger katika mchezo wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kuzuiwa na wasimamizi wa mechi.
    Taarifa ya Mkwasa kwa vyombo vya Habari leo imesema klabu imezuiwa kutumia jezi za SportPesa kwa sababu hazikusajiliwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAAGIZA YANGA KUFANYA UCHAGUZI HARAKA, MKWASA ATAJA SABABU ZA KUTOVAA JEZI ZA WADHAMINI JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top