• HABARI MPYA

  Thursday, May 24, 2018

  MWIGULU: TFF ILIPASWA KUISAIDIA YANGA IFANYE VIZURI KOMBE LA SHIRIKISHO ILI TUONGEZEWE NAFASI ZA KUSHIRIKI

  Na Rehema Lucas, DODOMA
  WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Lameck Nchemba amesema kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipaswa kuisaidia Yanga kuboresha kikosi chake kwa ajili ya hatu ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ili ifanye vizuri na kuitengenezea nchi uwezekano wa kuongeza nafasi ya kushiriki michuano hiyo. 
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online mjini Dodoma, Waziri Mwigulu ambaye pia ni Rais wa klabu ya Singida United amesema kwamba TFF ilitakiwa kuchukua wachezaji kutoka timu nyingine mfano  Simba, Singida United au Azam kuwaingiza Yanga wacheze michuano ya Kombe la Shirikisho kuiongezea nguvu timu hiyo ili ifanye vizuri kwenye michuano hiyo.
  Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Lameck (kushoto)  akiwa na Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' na mmiliki mtarajiwa, Mohammed Dewji (katikati) 

  “TFF wangefanya kama mwaka 1998, Yanga ilipopewa wachezaji wa timu nyingine kuimarisha kikosi chake kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Michuano hii ni faida kwa nchi kwa ujumla, Yanga ikifanya vizuri tutaongezewa timu za kushiriki,"amesema Waziri Mwigulu, ambaye pia inafahamika ni mpenzi na mwanachama wa Yanga.
  Pamoja na hayo, Waziri Mwigulu amesema kwamba timu za Tanzania zinapaswa kuanza kushirikiana wakati wa michuano ya Afrika ili kusaidiana kufanya vizuri katika michuano hiyo.
  Mwigulu akasema mchawi mwingine wa timu hizo katika michuano hiyo ni maandalizi ya zimamoto, kwani zimekuwa zikizipa uzito mechi za Ligi Kuu ya hapa kuliko michuano ya Afrika.
  "Nilishangazwa kuona maandalizi ya Timu ya Yanga katika michuano hiyo ni tofauti na jinsi walivyokuwa wanajiandaa na mchezo wa Ligi kuu dhidi ya Simba, kundi hili la Yanga wamepangwa na Gor Mahia, Rayon ni kundi ambalo wangekuwa watu wanaojipanga na kuwa na ushirikiano ulikuwa ni mwaka wa kuongeza timu katika nchini yetu kwenye michuano ya Afrika,"
  "Ninakuhakikishia kama timu ya Zambia ingekuwa imepangwa katika kundi hili, wanatinga Nusu Fainali katika michuano hii, yaani sisi tunaona ni kama burudani tu, lakini wanatakiwa wacheze kwa mikakati," amesema Mwigulu
  Yanga SC ipo Kundi D kwenye Kombe la Shirikisho na hadi sasa imekwishacheza mechi mbili bila ushindi, ikifungwa 4-0 na U.S.M. Alger mjini Algiers nchini Algeria kabla ya kutoa sare ya 0-0 na Rayon Sport ya Rwanda mjini hapa na mwezi ujao itakamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kwa kumenyana na Gor Mahia ya Kenya.
  Mwaka 1998 ilipoingia hatua hiyo, iliazimwa wachezaji watatu kuimarisha kikosi chake, Monja Liseki kutoka Simba, Alphonce Modest na Shaaban Ramadhani waliokuwa wanacheza kwa mkopo kutoka klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi na wote wakaenda kuwa na mchango mkubwa kwenye timu.
  Wakati huo huo TFF ikiitwa FAT, yaani Chama cha soka Tanzania ilikuwa chini ya Mwenyekiti, Alhaj Muhiddin Ndolanga, Makamu wake, Subira Mambo ambaye sasa ni marehemu na Katibu Mkuu, Alhah Ismail Aden Rage.  
  Na mwaka huu, Yanga inakabiliwa na mapungufu katika safu ya ulinzi katikati, viungo wote wa ulinzi na uchezeshaji na washambuliaji – lakini hadi sasa haijaongeza mchezaji hata mmoja kutokana na kukabiliwa na hakli ngumu ya kiuchumi.  
  Rais wa TFF ni Wallace Karia, Makamu wake Michael Wambura amefungiwa maisha kujihusisha na soka na Katibu wake ni Wilfred Kidau. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWIGULU: TFF ILIPASWA KUISAIDIA YANGA IFANYE VIZURI KOMBE LA SHIRIKISHO ILI TUONGEZEWE NAFASI ZA KUSHIRIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top