• HABARI MPYA

  Monday, May 28, 2018

  SIMBA SC YAMALIZA LIGI KWA HESHIMA, MAJI MAJI YAUNGANA NA NJOMBE MJI KUSHUKA DARAJA

  Na Mwandishi Wetu, SONGEA 
  SIMBA SC imefanikiwa kumaliza msimu kwa kupoteza mechi moja tu, baada ya sare ya 1-1 na wenyeji Maji Maji FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea. 
  Hiyo inakuwa sare ya tisa ya msimu, mechi nyingine Simba SC ikishinda 20 na kufungwa moja tu na Kagera Sugar mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli wiki iliyopita Uwanja wa Taifa. 
  Maji Maji FC leo walitangulia kwa bao la mshambuliaji Marcel Boniventusa Kaheza kabla ya kiungo kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima kusawazisha kwa penalti.
  Niyonzima aliyesajiliwa msimu huu kutoka kwa mahasimu wa jadi, Yanga alipoteza nafasi ya kuifungia bao la ushindi Simba baada ya mkwaju wake wa penalti kupanguliwa na kipa Hashim Mussa kipindi cha pili.

  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Ndanda FC imeshinda 3-1 dhidi ya Stand United Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na kunusurika kushuka daraja.
  Kagera Sugar imepata ushindi wa 2-1 mbele ya wenyeji, Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Samora, Tanzania Prisons imeilaza 1-0 Singida United Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mtibwa Sugar imetoka sare ya 0-0 na Mbeya City Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Mwadui FC imewapiga wenyeji, Njombe Mji FC 2-0 Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe na Mbao FC imetoka sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. 
  Kwa matokeo hayo, Simba SC inamaliza msimu na pointi 69 baada ya mechi zake 30, wakati Azam FC yenye pointi 55 za mechi 29 wapo nafasi ya pili mbele ya mabingwa wa msimu uliopita, Yanga SC wenye pointi 52 za mechi 29.
  Mechi kati ya Yanga na Azam FC inatarajiwa kufanyika kuanzia Saa 2:00 usiku wa leo Uwanja wa Taifa na ndiyo itakuwa ya kuamua mshindi wa pili wa msimu huu. Azam wanataka sare tu kumaliza nafasi ya pili, lakini Yanga wanahitaji ushindi ili kumaliza nyuma ya Simba wakibebwa na wastani wao mzuri wa mabao na pia kwa sababu walishinda mechi ya kwanza Chamazi.   
  Maji Maji na Njombe Mji FC ziimeshuka Daraja kutokana na tayari African Lyon, KMC, JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Alliance Schools ya Mwanza na Biashara United ya Mara zimekwishapanda kuelekea ligi ya msimu ujao, itakayokuwa na timu 20 ambayo ni ongezeko la timu nne.
  Simba SC, zamani ikijulikana kama Sunderland msimu huu imetwaa taji la 19 baada ya awali kubeba katika miaka ya 1965, 1966 (kama Sunderland), 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004, 2007, 2009–10 na 2011–2012.
  Lakini mahasimu wao, Yanga SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi wa Ligi Kuu, baada ya kubeba taji mara 27 katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2007–2008, 2008–2009, 2010–2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.
  Timu nyingine zilizowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ni Cosmopolitans 1967, Pan African 1982, Azam FC 2013-2014 zote za Dar es Salaam, Mseto SC 1975, Mtibwa Sugar 1999 na 2000 zote za Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986 na Coastal Union ya Tanga 1988.
  Kikosi cha Maji Maji kilikuwa; Hashim Mussa, Aziz Sibo, Mpoki Mwakinyuke, Juma Salamba, Kennedy Kipepe, Hassan Khamis, Peter Mapunda, Lucas Kikoti, Jerson Tegete, Marcel Kaheza na Jaffar Mohamed.
  Simba SC; Said Mohammed ‘Ndunda’, Ally Shomary, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Vincent Costa, Paul Bukaba, Muzamil Yassin/Kelvin Faru dk90, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Said Ndemla, Juma Luizio, Rashid Juma na Haruna Niyonzima.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAMALIZA LIGI KWA HESHIMA, MAJI MAJI YAUNGANA NA NJOMBE MJI KUSHUKA DARAJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top