• HABARI MPYA

    Wednesday, May 23, 2018

    TFF YAFUTA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA KIGENI LIGI KUU, 30 WATEULIWA KUWANIA ‘MPIRA WA DHAHABU’ 2108

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefuta tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo mwaka jana ilichukuliwa na kiungo Mzimbabwe wa Yanga, Thabani Scara Kamusiko – huku likiteua wachezaji 30 kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa ligi msimu wa 2017-2018. 
    Taarifa ya TFF iliyotolewa na Msemaji wa shirikisho hilo, Clifford Ndimbo imesema kwamba shere za Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu zitafanyika Juni 23 mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
    “Kufanyika kwa tuzo hizo ni utaratibu ambao Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limejiwekea kila mwaka baada ya kumalizika ligi kutoa tuzo kwa waliofanya vizuri kwa kushirikiana na Wadhamini wakuu wa VPL Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom Plc na msimu huu tutakuwa na washirika wengine Azam Tv, Benki ya KCB na Premier Bet,”amesema Ndimbo.

    Kiungo Mzimbabwe wa Yanga, Thabani Scara Kamusiko anakuwa mshindi wa mwisho wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni Ligi Kuu  

    Licha ya Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka wa ligi, pia kunatolewa tuzo mbalimbali, ambapo kwa mwaka huu tuzo moja imeondolewa na nyingine imeongezwa ikiwa ni katika kuboresha.
    Tuzo iliyoondolewa ni ya Mchezaji Bora wa Kigeni na imefanyika hivyo ili kuwapa fursa wachezaji wote kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL badala yakuwatenganisha.
    Pia msimu huu imongezwa Tuzo ya Mwamuzi Bora Msaidizi ambayo haikuwepo msimu uliopita, hiyo ni kutokana kuthamini nafasi ya waamuzi wasaidizi.
    Kwa mazingira hayo tuzo zitakazotolewa Juni 23, ambapo wadhamini wakuu ni Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ni hizi Bingwa, Mshindi wa Pili, Mshindi wa Tatu, Mshindi wa Nne, Mfungaji Bora, Timu yenye nidhamu, Mchezaji Bora chini ya umri wa miaka 20, aambayo imepewa jina la Tuzo ya Ismail Khalfan, Mchezaji Bora Chipukizi, Mwamuzi Bora Msaidizi, Mwamuzi Bora, Kipa Bora, Kocha Bora, Bao Bora Kikosi Bora cha Wachezaji 11 wa Ligi Kuu na Mchezaji wa Heshima.
    Zawadi kwa kila kategori pamoja na majina ya wanaowania tuzo ukiacha bingwa, mshindi wa pili, wa tatu, wa nne na mfungaji bora ambao hujulikana kulingana na ligi inavyoendelea zitatangazwa siku za usoni.
    Kamati ya Tuzo za VPL, imekamilisha orodha ya awali ya wachezaji 30 kwa ajili ya kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL msimu wa mwaka 2017/18, ambayo sherehe zake zitafanyika Juni 23 mwaka huu.
    Kila mwezi Kamati ya Tuzo, imekuwa ikitangaza jina la mchezaji aliyefanya vizuri kwa mwezi husika kutokana na vigezo mbalimbali na pia ripoti kutoka kwa makocha waliopo katika viwanja ambavyo ligi hiyo inachezwa.
    Wachezaji walioshinda tuzo za mwezi ligi ya msimu huu na miezi yao katika mabano nimshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (Agosti), beki wa Singida United, Shafiq Batambuze (Septemba) na mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa (Oktoba). Wengine ni kiungo wa Singida United, Mudathir Yahya (Novemba), mshambuliaji wa Mbao FC ya Mwanza, Habibu Kiyombo (Desemba), mshambuliaji wa Simba, John Bocco(Januari), kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi (Februari), mshambuliaji wa  Lipuli, Adam Salamba (Machi) na mshambuliaji wa Majimaji, Marcel Kaheza (Aprili).
    Wachezaji hao kila mmoja amepewa zawadi ya tuzo, king'amuzi cha Azam na fedha taslimu sh. Mil. Moja kutoka kwa wadhamini Vodacom.
    Hivyo wakati huu tukielekea mwisho wa ligi, leo tunatangaza wachezaji 30 ambao watawania tuzo hiyo, ambao watachujwa na kubaki 10, kisha watabaki watatu ambao ndiyo wataingia fainali ya kuwania tuzo siku ya mwisho.
    Wachezaji hao 30 ni Habibu Kyombo (Mbao FC), Khamis Mcha (Ruvu Shooting FC), Yahya Zayed (Azam FC), Razack Abalora (Azam FC), Bruce Kangwa (Azam FC), Aggrey Morris (Azam FC), Himid Mao (Azam FC), Awesu Awesu (Mwadui FC), Adam Salamba (Lipuli FC), Mohammed Rashid (Prisons FC), Shafiq Batambuze (Singida United) na Mudathir Yahya wa Singida United.
    Wengine ni Marcel Kaheza wa Maji Maji FC, Ditram Nchimbi wa Njombe Mji FC, Eliud Ambokile wa Mbeya City, Shaaban Nditi, Hassan Dilunga wote wa  wa Mtibwa Sugar, Tafadzwa Kutinyu wa Singida United, Ibrahim Ajib, Gardiel Michael, Papy Tshishimbi, Kelvin Yondani, Obrey Chirwa wote wa Yanga SC, Aishi Manula, Emmanuel Okwi, John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya na Asante Kwasi wote wa Simba SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAFUTA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA KIGENI LIGI KUU, 30 WATEULIWA KUWANIA ‘MPIRA WA DHAHABU’ 2108 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top