• HABARI MPYA

    Friday, May 25, 2018

    KARIA: TUTAFANYIA KAZI AGIZO LA RAIS DK. MAGUFULI KWA KUHAKIKISHA TIMU ZA TAIFA ZINAFANYA VIZURI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kwamba watafanyia kazi agizo la Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kutaka timu za nchini zifanye vyema kwenye mashindano ya kimataifa.
    Jumamosi Rais Dk. Magufuli wakati anawakabidhi Simba SC Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam wakitokwa kufungwa 1-0 na Kagera Sugar alisema kwamba Tanzania imefungwa vya kutosha kwenye mashindano ya kimataifa ya soka na umefika wakati ianze kushinda.
    Rais Magufuli alisema ni miaka mingi sasa tangu taifa limepata uhuru mwaka 1961, lakini timu za nchini zimekuwa hazifiki mbali kwenye mashindano na akaagiza ufike wakati timu zetu ziweze kushiriki Kombe la Afrika na kombe la Dunia.
    Na Alhamisi Rais wa TFF, Karia mwenye asili ya Somalia amesema; “Alichozungumza Mh.Rais Magufuli tumekipokea na tunaahidi tutakifanyia kazi kwa vitendo katika kuunga mkono jitihada zake za dhati kuona mpira wa miguu unapiga hatua,”. 

    Wallace Karia amesema watafanyia kazi agizo la Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli  

    Karia alisema watahakikisha wanasimamia mpira wa Tanzania kwa kuongozwa na sheria, kanuni na utaratibu na hawatakubali kuona mtu anakwenda kinyume na kutaka kuvuruga taswira nzuri ya mpira waliyoanza kuijenga katika kipindi kifupi tangu waingie madarakani. 
    “Tunaamini ushirikiano wetu na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mh.Rais John Pombe Magufuli tutafikia lengo kwa pamoja. Serikali ya awamu ya tano imekuwa na ushirikiano mkubwa na TFF katika kufanikisha masuala mbalimbali ushirikiano ambao hakika utaleta matunda zaidi,” aliongeza. 
    Karia alisema wanaamini timu zetu za Taifa zitafanya vizuri kama ambavyo timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ilivyofanya vizuri na kuchukua Kombe la CECAFA Challenge nchini Burundi na timu ya wasichana ya kituo cha TSC nao ilivyofanya vizuri na kufika fainali ya Kombe la dunia la Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini Urusi katikati ya mwezi huu. 
    Hata hivyo, katika taarifa yake Karia hakuzungumzia kutolewa mapema kwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes kwenye michuano ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U20) mwakani nchini Niger.

    Jumamosi Rais Dk. John Magufuli amesema inatosha Tanzania kufungwa kwenye mashindano ya kimataifa 

    Ngorongoro Heroes, ikiwa chini ya kocha Ammy Ninje ilitupwa nje ya michuano hiyo kwa kufungwa jumla ya mabao 6-2, ikichapwa 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kutandikwa 4-1 mjini Bamako.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA: TUTAFANYIA KAZI AGIZO LA RAIS DK. MAGUFULI KWA KUHAKIKISHA TIMU ZA TAIFA ZINAFANYA VIZURI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top