• HABARI MPYA

  Monday, May 28, 2018

  SIMBA SC YAIMARISHA KIKOSI KWA KUSAJILI ‘MASHINE MBILI ZA NGUVU’

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kusajili chipukizi wawili, Adam Salamba na Marcelo Boniventura Kaheza huku pia ikiwa mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji mwingine anayechipukia, Mohammed Rashid.
  Wakati Salamba ametambulishwa rasmi leo baada ya kusaini na Rais wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’ akishuhudiwa na mfadhili, Mohammed ‘Mo’ Dewji, Kaheza amekiri mwenyewe kusaini Simba.
  Baada ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu akiisaidia Maji Maji kupata sare ya 1-1 na Simba Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Kaheza akawaambia Waandishi wa Habari kwamba amesaini Simba.

  Mfadhili wa Simba SC, Mohammed Dewji (katikati) akiwa na mshambuliaji, Adam Salamba (kushoto) baada ya mchezaji huyo kusaini mkataba wa kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi kutoka Lipuli ya Iringa 
  Hapa Adam Salamba (kushoto) akisaini mkataba wa kujiunga na Simba mbele ya Rais, Salim Abdallah 'Try Again' 

  Na kwa kusaini Simba, maana yake Kaheza anarejea nyumbani kwani mchezai huyo aliibukia timu ya vijana ya Wekundu wa Msimbazi kabla ya kwenda kuamua kutafuta timu atakazokuwa anacheza kwa muda mrefu kupata uzoefu.
  Na baada ya kufunga maba 14 msimu huu katika Ligi Kuu, akimfuatia mshambuliaji wa Simba SC,Mganda Emmanuel Okwi aliyefunga mara 20– Kaheza ameivutia tena timu yake ya zamani ambayo imeamua kumrejesha.
  Aidha, wakati Simba ikimtambulisha Salamba leo mjini Dar es Salaam, taarifa zaidi zinasema chipukizi mwingine, Mohammed Rashid atakamailisha mambo Msimbazi wakati wowote.         
  Simba SC imefanikiwa kumaliza msimu kwa kupoteza mechi moja tu, baada ya sare ya 1-1 na wenyeji Maji Maji FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea. 
  Hiyo inakuwa sare ya tisa ya msimu, mechi nyingine Simba SC ikishinda 20 na kufungwa moja tu na Kagera Sugar mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli wiki iliyopita Uwanja wa Taifa. 
  Maji Maji FC leo walitangulia kwa bao la mshambuliaji Marcel Boniventusa Kaheza kabla ya kiungo kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima kusawazisha kwa penalti.
  Niyonzima aliyesajiliwa msimu huu kutoka kwa mahasimu wa jadi, Yanga alipoteza nafasi ya kuifungia bao la ushindi Simba baada ya mkwaju wake wa penalti kupanguliwa na kipa Hashim Mussa kipindi cha pili.
  Kwa matokeo hayo, Simba SC inamaliza msimu na pointi 69 baada ya mechi zake 30, wakati Azam FC yenye pointi 55 za mechi 29 wapo nafasi ya pili mbele ya mabingwa wa msimu uliopita, Yanga SC wenye pointi 52 za mechi 29.
  Simba SC, zamani ikijulikana kama Sunderland msimu huu imetwaa taji la 19 baada ya awali kubeba katika miaka ya 1965, 1966 (kama Sunderland), 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004, 2007, 2009–10 na 2011–2012.
  Lakini mahasimu wao, Yanga SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi wa Ligi Kuu, baada ya kubeba taji mara 27 katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2007–2008, 2008–2009, 2010–2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.
  Timu nyingine zilizowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ni Cosmopolitans 1967, Pan African 1982, Azam FC 2013-2014 zote za Dar es Salaam, Mseto SC 1975, Mtibwa Sugar 1999 na 2000 zote za Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986 na Coastal Union ya Tanga 1988.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAIMARISHA KIKOSI KWA KUSAJILI ‘MASHINE MBILI ZA NGUVU’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top