• HABARI MPYA

  Saturday, May 26, 2018

  AZAM FC YATHIBITISHA KUMCHUKUA DONALD NGOMA, YAMPELEKA AFRIKA KUSINI KWANZA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Azam FC umethibitisha kuingia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji Donald Ngoma, kwa ajili ya msimu ujao 2018/2019.
  Baada ya kuingia makubaliano hayo, muda wowote kuanzia sasa Azam FC inatarajia kumpeleka mchezaji huyo katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kumfanyia vipimo vya afya ili kuona ni kwa kiasi gani majeraha yaliyokuwa yakimsumbua yamepona.
  Azam FC inaamini ya kuwa ujio wa nyota huyo kutoka nchini Zimbabwe aliyewahi kuchezea FC Platinum ya huko kabla ya kuhamia Yanga, ni sehemu tu ya mikakati ya benchi la ufundi na uongozi katika kuboresha kikosi kwenye eneo la ushambuliaji kuelekea msimu ujao.

  Donald Ngoma akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Asam FC, Abdulkarim Amin 'Popat'

  Aidha kama mambo yataenda vizuri, uongozi wa Azam FC unaamini kuwa Ngoma atakuwa ni miongoni mwa nyota wapya wa timu hiyo watakaoonekana kwenye kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame.
  Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Julai na Azam FC ndiyo mabingwa watetezi.
  Tayari mchezaji huyo ameandaliwa jezi namba 11 iliyokuwa ikitumiwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, aliyerejea Aduana Stars ya nchini kwao Ghana.
  "Tunawaomba mashabiki wetu wa Azam FC wawe watulivu katika kipindi hiki na kuendelea kuisapoti timu, kwani uongozi umejipanga kufanyia kazi ripoti ya benchi ya ufundi na kuboresha kikosi ili kusaka taji la ubingwa msimu ujao," imesema taarifa ya Azam FC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YATHIBITISHA KUMCHUKUA DONALD NGOMA, YAMPELEKA AFRIKA KUSINI KWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top