• HABARI MPYA

  Thursday, May 31, 2018

  BOCCO, OKWI, MAVUGO NA WAGHANA WOTE HAWAMO SIMBA KIKOSI CHA SPORTPESA KENYA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  VINARA wa mabao wa Simba SC, Nahodha John Raphael Bocco na Mganda Emmanuel Arnold Okwi wote hawamo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichiokwenda kwenye Kenya kwenye michuano ya SportPesa Super Cup.
  Pamoja hao, kwenye kikosi hicho wanakosekana pia beki Mganda, Juuko Murshid, mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo na Waghana wote, beki Asante Kwasi na kiungo mshambuliaji, Nicholaus Gyan anayetumika kama mlinzi pia kwa sasa.
  Kikosi cha Simba SC kilichoondoka leo asubuhi kwenda Kenya kinaundwa na makipa; Aishi Manula na Said Mohamed ‘Nduda’, mabeki Ally Salim, Ally Shomary, Paul Bukaba, Erasto Nyoni, Yussuf Mlipili, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

  Nahodha John Raphael Bocco hayumo kwenye kikosi cha Simba SC kilichokwenda Kenya 

  Wengine ni viungo Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Muzamil Yassin, Said Hamisi Ndemla, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya na Mohamed ‘Mo’ Ibrahim wakati washambuliaji ni Moses Kitandu na Rashid Juma.
  Simba pia imemchukua mshambuliaji wake mpya, Marcel Boniventura Kaheza iliyemsajili kutoka Maji Maji ya Songea, ingawa kanuni za mashindano haziruhusu wachezaji wapya. 
  Simba SC wanatarajiwa kufungua dimba na Kariobangi Sharks Jumapili kabla ya mahasimu wao wa jadi, Yanga kuvaana na Kakamega Homeboys Jumatatu 4, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Afraha, Nakuru.
  Mabingwa watetezi, Gor Mahia wao pia wataanza na JKU Jumapili, wakati Singida United itaanza na AFC Leopards Jumanne. 
  Ikumbukwe bingwa wa michuano hiyo ataondoka kitita cha dola za Kimarekani, 30,000, mshindi wa pili dola 10,000, wa tatu dola 7,500 zitakazoishia Nusu Fainali dola 5,000 na za Robo Fainali dola 2,500.
  Pamoja na dola 30,000, bingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu atapata fursa ya kwenda kumenyana na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Walton, Liverpool nchini England.
  Mwaka jana Gor Mahia ilikuwa bingwa wa kwanza wa michuano hiyo baada ya kuwafunga mahasimu wao, AFC Leopard 2-1 katika fainali kwenye michuano iliyofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BOCCO, OKWI, MAVUGO NA WAGHANA WOTE HAWAMO SIMBA KIKOSI CHA SPORTPESA KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top