• HABARI MPYA

    Tuesday, May 22, 2018

    YANGA YAFUTA GUNDU, YAICHAPA 1-0 MBAO FC USHINDI WA KWANZA NDANI YA MECHI 10

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imefuta mkosi, baada ya kushinda mechi ya kwanza tangu ikimbiwe na aliyekuwa kocha wake, Mzambia George Lwandamina kufuatia kuilaza 1-0 Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Shukrani kwake mfungaji wa bao hilo la kwanza la Yanga ndani ya mechi saba mdululizo, kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko aliyemtungua kwa shuti la mpira wa adhabu, kipa Metacha Boniphace Mnata anayedaka kwa mkopo kutoka Azam FC dakika ya 26.
    Refa Abubakar Mturo kutoka Mtwara aliwapa Yanga nafasi ya kupiga mpira wa adhabu nje kidogo ya boksi,baada ya beki wa Mbao FC, David Mwasa kuunawa mpira na rasta Mzimbabwe akatumia makosa ya Mnata kusimama nyuma ya ukuta wa mabeki wake kumtungua kwa urahisi.
    Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh (kulia) akifurahia na wachezaji wake baada ya mechi leo. Katikati ni mfungaji wa bao pekee la ushindi, Thabani Kamusoko

    Thabani Kamusoko akimtoka mchezaji wa Mbao FC leo Uwanja wa Taifa
    Mshambuliaji wa Yanga, Matheo Anthony (kushoto) akijivuta kupiga shuti mbele ya mabeki wa Mbao
    Kiungo wa Yanga SC, Paul Godfrey akiruka miguu yaq beki wa Mbao FC, Amos Charles 

    Yanga iliendelea kutengeneza nafasi nzuri kwa mashambulizi ya kupitia katikati, lakini tatizo likawa kwenye umaliziaji na haikuwa ajabu dakika 90 na ushei za mchezo zikamalizika bila mabao zaidi.
    Kwa Ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 51 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 55 za mechi 29 na mabingwa tayari, Simba SC wenye pointi 68 za mechi 29.
    Yanga SC itamenyana na Ruvu Shooting Ijumaa wiki hii, kabla ya kukutana na Azam FC katika mchezo wa mwisho wa msimu Jumatatu, mechi zote Uwanja wa Taifa mjini hapa.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Said Makapu, Shaibu Abdallah, Maka Edward, Pius Buswita, Emmanuel Martin, Yusufu Mhilu/Matheo Anthony dk51, Raphael Daudi/Paul Godfrey dk76 na Thaban Kamusoko
    Mbao FC; Matacha Mnata, Vicent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Chitembe Babilas, Yusufu Ndikumana, Boniface Maganga/Ismail Ally dk55, Ally Kombo, Rajesh Kotecha, Emmanuel Mbuyekure na Ndaki Robert/Kelvin Kijiri dk55.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAFUTA GUNDU, YAICHAPA 1-0 MBAO FC USHINDI WA KWANZA NDANI YA MECHI 10 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top