• HABARI MPYA

  Tuesday, May 22, 2018

  MBEYA CITY YAWA KAMPUNI YA HISA…YAANZA NA MTAJI WA SH. BILIONI 100

  Na Doreen Mwambenja, MBEYA
  WAMILIKI wa Mbeya City FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Halmashauri ya jiji la Mbeya imebadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo na sasa ni Kampuni.
  Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo mjini hapa.
  Kimbe amesema kwamba kampuni hiyo ambayo imesajiliwa Januari 26, mwaka huu na Msajili wa Makampuni na Biashara (BRELA) chini ya sheria ya makampuni ya mwaka 2002, inaitwa Mbeya City Football Club Public Limited Company (Mbeya City FC PLC) kwa hati namba 140785 na imesajiliwa pia na Posta Mbeya kwa anuani namba 663.
  Kimbe amesema kwamba Mbeya City FC PLC inatarajia kukusanya mtaji wa Shilingi Bilioni 100 ili kujiendesha kwa ufanisi.

  Mtendaji Mkuu wa Mbeya City FC, Emmanuel Kimbe (kushoto) amesema klabu sasa inakuwa kampuni

  “Katika mfumo huu, Halmashauri ambaye ni mmiliki ataamua ni sehemu gani (asilimia) ya hisa atakazobaki nazo na nyingine zitapelekwa kwenye soko la mitaji ili kutafuta wamiliki/wabia wengine. Hisa hizo zitakuwa wazi kwa watu wote waliopo ndani na nje ya nchi,”imesema taarifa ya Kombe na kuongeza; 
  “Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni na Menejimenti ya timu itaundwa upya baada ya wanahisa wote kupatikana,”amesema. 
  Kimbe amesema lengo la mabadiriko hayo ya kihistoria ni kufungua mlango wa kupata wabia watakaoweza kukuza mtaji wa kampuni ili kufanya uwekezaji mkubwa kwenye timu, kugharamia miradi itakayojikita katika maendeleo ya mpira wa miguu na miradi mingine itakayochochea ukuaji wa uchumi wa kampuni na taifa kwa ujumla.
  “Klabu inapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wadau na wananchi mbalimbali walioiunga mkono katika kipindi chote hicho toka timu imeanzishwa mwaka 2011 na inawakaribisha kumiliki klabu yao pendwa kupitia utaratibu wa HISA pindi taratibu za uuzwaji wa hisa hizo utakapokamilika mapema katika siku za usoni na  kuandikishwa katika Soko la Mitaji la Dar Es Salaam (DSE),”.
  Mbeya City inakuwa klabu ya pili nchini kujaribu kujiendesha kama Kampuni, baada ya Yanga SC mwaka 2001, ambayo hata hivyo ilishindikana baada ya baadhi ya wanachama wake kwenda mahakamani kupinga.
  Lakini pia Mbey City inajaribu kufuata nyayo za Simba SC, ambayo yenyewe ni juzi tu wanachama wake walipitisha Katiba mpya katika mkutano uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam, inayobadili mfumo wa uendeshwaji wake na kuwa ya kuuza hisa.
  Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama 1,000 na ushei ukiongozwa na Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, marekebisho ya Katiba ya Simba SC yamepita kwa kishindo, wanachama watatu tu wakinyoosha mikono kupinga.
  Katika marekebisho hayo, Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC chini ya Mwenyekiti ambaye pia atakuwa Rais wa klabu, atatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha Shahada sawa na Wajumbe wake wawili wa kuchaguliwa – na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wawili, mmoja mwanamke.
  Kupitishwa kwa mabadiliko ya katiba ndani ya Simba kunafungua milango ya mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji kuwa mwanahisa mkuu wa klabu.
  Hiyo ni baada ya Mo Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
  Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
  Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBEYA CITY YAWA KAMPUNI YA HISA…YAANZA NA MTAJI WA SH. BILIONI 100 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top