• HABARI MPYA

  Friday, May 25, 2018

  ULIMWENGU AREJEA AFRIKA KUJIPANGA UPYA, AJIUNGA NA EL HILAL YA SUDAN

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesaini mkataba wa kujiunga na klabu yake ya El Hilal ya Sudan baada ya kuachana na AFC Eskilstuna ya Sweden.
  Ulimwengu anarejea uwanjani baada ya kupona maumivu ya goti kufuatia kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini mwaka jana na kupitia kipindi kirefu cha mazoezi ya kujiweka fiti.
  Ulimwengu alikwenda kwa watalaamu nchini Italia kufanyishwa mazoezi maalum ya kumuweka fiti haraka arejee uwanjani, ambayo hakika yamemsaidia na sasa anajiunga na vigogo wa Sudan wanaoongoza Ligi ya kwao.
  Thomas Ulimwengu akisaini mkataba wa kujiunga na El Hilal ya Sudan jana
  Maumivu ya goti yamekuwa yakimsakama Ulimwengu tangu alipojiunga na Eskilstuna Januari mwaka jana akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kiasi cha kushindwa kucheza. 
  Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011  alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
  Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
  Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU AREJEA AFRIKA KUJIPANGA UPYA, AJIUNGA NA EL HILAL YA SUDAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top