• HABARI MPYA

  Tuesday, May 22, 2018

  YANGA SC YATAFUTA USHINDI WA KWANZA KATIKA MECHI 10 LEO IKITOKA KUFUNGWA TANO, SARE NNE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC leo itajaribu kusaka ushindi wa kwanza ndani ya mechi 10 itakapomenyana na Mbao FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Japokuwa bingwa wa Ligi Kuu amekwishapatikana Simba SC, lakini Yanga wanatafuta heshima ya kumaliza nafasi ya pili na Mbao FC wanapambana kuepuka kushuka Daraja – na hapo ndipo ulipolalia utamu wa mchezo wa leo.
  Lakini hali ya kujiamini imetoweka kwa wachezaji na hata benchi la Ufundi Yanga kufuatia timu kucheza mechi tisa bila ushindi tangu iachwe na aliyekuwa kocha wake Mkuu, Mzambia George Lwandamina Aprili 9, mwaka huu.
  Yanga SC leo inasaka ushindi wa kwanza ndani ya mechi 10 itakapomenyana na Mbao FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam 


  REKODI YA YANGA SC TANGU AONDOKE LWANDAMINA  

  Aprili 11, 2018; Yanga 1-1 Singida United (Ligi Kuu Dar es Salaam)

  Aprili 18, 2018; Welayta Dicha 1-0 Yanga SC (Kombe la Shirikisho)

  Aprili 22, 2018; Mbeya City 1-1 Yanga SC (Ligi Kuu Mbeya)

  Aprili 29, 2018; Simba 1 – 0 Yanga SC (Ligi Kuu Dar es Salaam)

  Mei 6, 2018; USM Alger 4-0 Yanga SC (Kombe la Shirikisho Algiers)

  Mei 10, 2018; Tanzania Prisons 2-0 Yanga SC (Ligi Kuu Mbeya)

  Mei 13; 2018; Mtibwa Sugar 1-0 Yanga SC (Ligi Kuu Morogoro)

  Mei 16, 2018; Yanga SC 0-0 Rayon Sports (Kombe la Shirikisho Dar es Salaam)

  Mei 19, 2018; Yanga SC 0-1 Mwadui FC (Ligi Kuu Shinyanga)

  Mei 22, 2018; Yanga SC Vs Mbao FC (Ligi Kuu Dar es Salaam)

  Lwandamina aliiongoza Yanga kushinda kwa mara ya mwisho Aprili 7,  ilipoichapa 2-0 Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.  
  Na baada ya kuondoka timu imefungwa mechi tano na kutoa sare nne hadi sasa, ikiwa chini ya waliokuwa Wasaidizi wake, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazalendo, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali wote wachezaji wa zamani wa klabu.
  Lakini tayari klabu imeleta kocha Mkuu mpya, Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambaye mwishoni mwa wiki alisaini mkataba wa miaka miwili na kurejea kwao, Kinshasa kabla ya kurudi mapema Juni kuanza rasmi kazi.  
  Kwa sasa Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu kwa pointi zake 48 za mechi 27, nyuma ya Azam FC wenye pointi 55 za mechi 29 na mabingwa, Simba SC wenye pointi 68 za mechi 29, wakati Tanzania Prisons yenye pointi 45 za mechi 29 inashika nafasi ya nne.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YATAFUTA USHINDI WA KWANZA KATIKA MECHI 10 LEO IKITOKA KUFUNGWA TANO, SARE NNE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top