• HABARI MPYA

  Monday, May 28, 2018

  AZAM FC YAIPIGA YANGA 3-1 NA KUMALIZA NAFASI YA PILI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imefanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wa 2017 – 2018 baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya mabingwa wa msimu uliopita, Yanga SC usiku huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo umetokana na mabao ya washambuliaji chipukizi wa timu hiyo, Yahya Zaid dakika ya nne Shaaban Idd Chilunda dakika ya 60 na kiungo mkongwe, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 68, wakati bao pekee la Yanga, Azam FC waklijifunga kupitia kwa beki wao, Abdallah Heri dakika ya 49. 
  Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza msimu na pointi 58 nyuma ya mabingwa, Simba SC waliomaliza na pointi 69, wakati Yanga SC wanabaki na pointi zao 52.
  Mshambuliaji wa Azam FC, Shaaban Iddi Chilunda akishangilia baada ya kufunga bao zuri la pili leo 
  Mshambuliaji wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa akipasua katikati ya wachezaji wa Azam FC
  Beki wa Yanga, Hassan Kessy akimpita kiungo wa Azam FC, Joseph Mahundi
  Shaaban Iddi akibinuka tik tak kuifungia Azam FC bao zuri la pili

  Mfungaji wa bao pekee la Yanga leo, beki wa Azam FC Abdallah Kheri (kulia) akiwahi mpira dhidi ya kiungo Mkongo wa wapinzani wao, Papy Kabamba Tshishimbi

  Msimu wa 2017-2018 umekamilishwa leo, Maji Maji na Njombe Mji FC wakiipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu na tayari African Lyon, KMC, JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Alliance Schools ya Mwanza na Biashara United ya Mara zimekwishapanda kuelekea ligi ya msimu ujao, itakayokuwa na timu 20 ambayo ni ongezeko la timu nne.
  Simba SC, zamani ikijulikana kama Sunderland msimu huu imetwaa taji la 19 baada ya awali kubeba katika miaka ya 1965, 1966 (kama Sunderland), 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004, 2007, 2009–10 na 2011–2012.
  Lakini mahasimu wao, Yanga SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi wa Ligi Kuu, baada ya kubeba taji mara 27 katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2007–2008, 2008–2009, 2010–2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.
  Timu nyingine zilizowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ni Cosmopolitans 1967, Pan African 1982, Azam FC 2013-2014 zote za Dar es Salaam, Mseto SC 1975, Mtibwa Sugar 1999 na 2000 zote za Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986 na Coastal Union ya Tanga 1988.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Abdalah Shaibu ‘Ninja’, Said Juma ‘Makapu’, Maka Edward, Pius Buswita, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Matheo Anthony na Thabani Kamusoko.
  Azam FC; Razack Abalora, Abdul Hajji, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo, Shaaban Iddi, Yahya Zayed na Joseph Mahundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAIPIGA YANGA 3-1 NA KUMALIZA NAFASI YA PILI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top