• HABARI MPYA

    Friday, May 25, 2018

    YANGA SC NA AZAM FC KUMENYANA USIKU KUWANIA NAFASI YA PILI LIGI KUU JUMATATU TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara litafungwa usiku wa Jumatatu ya Mei 28, mwaka huu kwa mchezo kati ya Yanga SC na Azam FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Taarifa ya Mkurugenzi wa Bodi wa Ligi, Boniphace Wambura Mgoyo kwa vyombo vya Habari leo imesema kwamba mchezo huo utaanza Saa 2:00 usiku.
    Wambura amesema kwamba mechi nyingine zote za kufunga pazi la Ligi Kuu msimu 2017- 2018 zitachezwa kuanzia Saa 10: 00 jioni Jumatatu ya Mei 28, 2018 kwa timu zote 16 kuingia viwanjani kukamilisha raundi ya 30 na mechi 240 za msimu huu.
    Wambura, Ofisa wa zamani wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa (TPBC) amezitaja mechi hizo ni kati ya Maji Maji ya Songea na mabingwa, Simba SC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Lipuli na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba na Tanzania Prisons dhidi ya Singida United Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

    Mechi nyingine ni kati ya Ndanda FC dhidi ya Stand United Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Mtibwa Sugar dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro, Njombe Mji FC dhidi ya Mwadui FC na Mbao FC dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Wakati Ligi Kuu inamalizika Jumatatu, tayari Simba SC ndiyo mabingwa wakiwa wamejikusanyia pointi 68 katika mechi 29, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 55 za mechi 29 na waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 51 za mechi 28 na leo wanacheza mechi yao ya 29 dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa.
    Njombe Mji FC tayari imeshuka Daraja kutokana na kuambulia pointi 22 katika mechi 29, wakati Ndanda FC yenye pointi 26 za mechi 29 na Maji Maji FC yenye pointi 24 za mechi 29 pia mojawapo itashuka pia baada ya mechi za Jumatatu.
    Wakati timu mbili zitaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu Jumatatu, tayari African Lyon, KMC, JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Alliance Schools ya Mwanza na Biashara United ya Mara zimekwishapanda kuelekea ligi ya msimu ujao, itakayokuwa na timu 20 ambayo ni ongezeko la timu nne.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC NA AZAM FC KUMENYANA USIKU KUWANIA NAFASI YA PILI LIGI KUU JUMATATU TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top