• HABARI MPYA

  Thursday, May 31, 2018

  MICHUANO YA KOMBE LA KAGAME KUFANYIKA SAMBAMBA NA KOMBE LA DUNIA MWEZI HUU DAR

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA Kagame itafanyika mjini Dar es Salaam, Tanzania sambamba na Fainali za Kombe la Dunia mwezi huu nchini Urusi.
  Kwa kawaida katika mwezi wa Fainali za Kombe la Dunia, wenye mpira wao, FIFA huagiza yasifanyike mashindano mengine yoyote.
  Lakini Bin Zubeiry Sports – Online inafahamu kwamba FIFA chini ya Rais wake, Giovanni Vincenzo ‘Gianni’ Infantino, Mswisi mwenye asili ya Italia imeikubalia CECAFA, Baraza la Vyama  vya Soka Afrika Mashariki na Kati kufanya mashindano hayo mwezi huu.

  Kagame ya 2015 ndiyo ilimtoa Michael Olunga ambaye kwa sasa anachezea Girona FC ya Hispania  

  Hiyo ni kwa sababu washiriki watano wa michuano hiyo wapo kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, ambayo kwa sasa imesimama kupisha Kombe la Dunia itarejea Julai baada ya kumalizika kwa michuano hiyo nchini Urusi.

  Hao ni KCCA ya Uganda iliyopo Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine nne kwenye Kombe la Shirikisho ambazo ni Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda, Yanga ya Tanzania zilizopoi Kundi D zote na Al-Hilal ya Sudan iliyopo Kundi A.
  Na kwa sababu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika itakwenda hadi Agosti, mwezi ambao msimu mpya wa Ligi Kuu nyingi duniani huanza – michuano ya Kagame isipofanyika mwezi huu kuna hatari isifanyike tena na mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo.
  Azam FC ndiyo mabingwa wa mwisho wa michuano hiyo ilipofanyika Tanzania, walipowafunga Gor Mahia 2-0 katika fainali Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya waliokuwa washambuliaji wake hatari, John Raphael Bocco dakika ya 17 na Muivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 64.
  Na hiyo ndiyo ilikuwa michuano iliyomtoa mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga ambaye kwa sasa anachezea Girona FC ya Hispania kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China.
  Baada ya kufungha mabao matano akiwa na Gor Mahia na kuibuka mfungaji bora akiwapiku , Osman Bilal Salaheldin wa Al-Khartoum ya Sudan aliyefunga mabao manne sawa na Tchetche wa Azam FC, Olunga akachukuliwa na Djurgardens IF ya Sweden mwaka 2016 iliyomuuza Guizhou Zhicheng mwaka 2017.
  Na Tanzania itawakilishwa na Azam FC kama mabingwa watetezi wa mashindano na Yanga SC, kama mabingwa wa nchi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MICHUANO YA KOMBE LA KAGAME KUFANYIKA SAMBAMBA NA KOMBE LA DUNIA MWEZI HUU DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top