• HABARI MPYA

  Wednesday, May 30, 2018

  KIUNGO CHIPUKIZI YANGA, MAKA EDWARD AMVULIA MCHEZAJI MPYA JEZI NAMBA 8

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAKATI kikosi cha Yanga SC kinaondoka kesho mjini Dar es Salaam kwenda Kenya kwa ajili ya michuano ya SportPesa Super Cup, kiungo chipukizi Maka Edward amesema hatatumia jezi namba 8 kuanzia sasa kwa sababu anamuachia mchezaji mpya.
  Hata hivyo, Maka hajamtaja jina mchezaji huyo mpya ajaye katika sehemu ndogo ya video iliyopostiwa kwenye akaunti rasmi ya Instagram, ya klabu ingawa miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwa mbioni kusajiliwa ni kiungo mshambuliaji, Mrisho Khalfan Ngassa.
  Kama ni Ngassa, ambaye kwa sasa anachezea Ndanda FC ya Mtwara atakuwa anajiunga na Yenga kwa mara ya tatu baada ya awali kuchezea kwa awamu mbili na kwa mafanikio.
  Maka Edward amesema hatatumia jezi namba 8 kuanzia sasa kwa sababu anamuachia mchezaji mpya 


  Ngassa alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwazna mwaka 2006 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba na akadumu hadi 2010 alipohamia Azam FC ya Dar es Salaam pia, ambako alidumu 2013 alipotolewa kwa mkopo Simba SC.Ngassa alirejea Yanga SC mwaka 2013 na akacheza hadi mwaka 2015 alipohamia Free State Stars ya Afrika Kusini ambako alicheza kwa msimu mmoja na nusu.
  Mwaka 2016 alikwenda Fanja ya Oman ambako alidumu kwa mwezi mmoja kabla ya kurudi nyumbani kujiunga na MbeyA City alikocheza kwamwaka mmoja kabla ya Januari mwaka huu kuhamia Ndanda FC.
  Kikosi cha wachezaji 20 wa Yanga, wakiwemo Nahodha Kevin Yondan, kiungo Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kinaondoka kesho kwenda Kenya kwa ajili ya michuano ya pili ya SportPesa Super Cup. 
  Katika michuano hiyo inayoanzia hatua ya Robo Fainali, Yanga wataanza na Kakamega Homeboys Juni 4, siku moja baada ya majasimu wao, Simba SC kumenyana na dimba na Kariobangi Sharks Juni 3 na, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Afraha, Nakuru.
  Mechi nyingine ni kati ya mabingwa watetezi, Gor Mahia na JKU ya Zanzibar Juni 3 pia na Singida United ya Singida dhidi ya wenyeji wengine, AFC Leopards Juni 5. 
  Ikumbukwe bingwa wa michuano hiyo ataondoka kitita cha dola za Kimarekani, 30,000, mshindi wa pili dola 10,000, wa tatu dola 7,500 zitakazoishia Nusu Fainali dola 5,000 na za Robo Fainali dola 2,500.
  Pamoja na dola 30,000, bingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu atapata fursa ya kwenda kumenyana na klabu ya Everton nchini England.
  Mwaka jana Gor Mahia ilikuwa bingwa wa kwanza wa michuano hiyo baada ya kuwafunga mahasimu wao, AFC Leopard 2-1 katika fainali kwenye michuano iliyofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIUNGO CHIPUKIZI YANGA, MAKA EDWARD AMVULIA MCHEZAJI MPYA JEZI NAMBA 8 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top