• HABARI MPYA

  Monday, May 28, 2018

  NEYMAR ASEMA BADO HAJISIKII VIZURI SANA, LAKINI ATACHEZA

  MSHAMBULIAJI Neymar amesema kwamba hayuko fiti kwa asilimia 100 baada ya mazoezi ya wiki moja na kikosi cha timu yake ya taifa, Brazil kujiandaa kwa Fainali za Kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi.
  Mshambuliaji huyo amesema kwamba bado hajisikii vizuri sana katika mguu wake wa kulia ulioumia, lakini anaamini atakuwa vizuri kwa mashindano nchini Urusi ambayo yataanza Juni 14. 
  “Niko vizuri, mguu wangu upo vizuri. Naweza vitu vichache. Bado sijisikii vizuri sana, lakini si kitu ambacho kitanisumbua,”amesema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, Neymar akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya Shirikisho la Soka Brazil mjini Rio de Janeiro.

  Neymar amesema hayuko fiti kwa asilimia 100 baada ya mazoezi ya wiki moja na Brazil kujiandaa kwa Fainali za Kombe la Dunia PICHA ZAIDI GONGA HAPA  

  Alipoulizwa anajisikia vizuri kiasi gani, Neymar alijibu: “Si asilimia 100 tayari. Lakini hiyo inakuja na muda. Ni kawaida kwamba nina woga wa kufanya vitu kikamilifu. Acha tuichukulie polepole, bado kuna siku nyingi hadi (Kombe la Dunia) kufunguliwa na nitakuwa fiti kwa asilimia 100,”alisema. 
  Neymar hajacheza mechi yoyote tangu Februari, lakini anatumai kuwa uwanjani tena katika mchezo wa kirafiki wa Brazil dhidi ya Croatia Juni 3 mjini Liverpool. “Niko tayari kucheza, hakuna cha kunizuia,”alisema. “Ninavyojisikia leo ni huu woga, kwa sababu ndiyo ninarejea sasa,”.
  Mbrazil huyo alilazimika kuondoka uwanjani baada ya kuumia kwenye mechi ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia nyumbani mwaka 2014 wakishinda 2-1 dhidi ya Colombia.
  Kikosi cha wachezaji 20 wa Brazil kimeondoka leo kwenda London kuendelea na maandalizi yao ya Kombe la Dunia baada ya wiki ya mazoezi katika kambi yao ya Granja Comary mjini Teresopolis, nje ya mji Rio na Neymar ameendelea kuimarika – akitembea na mpira na kutoa pasi kwa kasi. 
  Benchi la Ufundi la Brazil linajaribu kupunguza presha kwa nyota huyo kwa kusema itachukua muda hadi aanze kucheza katika ubora wake.
  Aidha, Neymar pia amekanusha habari za kuondoka Paris Saint-Germain baada ya kuulizwa, akijibu “Mtazamo wangu ni Brazil, watu wanasema mambo yasiyo na maana na hayo si ya kujibu,”.
  Washindi wa taji la Ligi la Mabingwa Ulaya, Casemiro na Marcelo wa Real Madrid na washindi wa pili wa michuano huyo, Roberto Firmino wa Liverpool watajiunga na kikosi Jumatano.
  Msemaji wa Shirikisho la Soka Brazil, Vinicius Rodrigues amesema kwamba kocha Tite ameamua kuwapa wachezaji hao watatu muda zaidi wa kupumzika kabla ya kujiunga na timu.
  Kikosi cha Brazili kitawasili leo Uwanja wa Ndege wa London Stansted baada ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tom Jobim mjini Rio na kitakapowasili England kitakuwa chini ya uenyeji wa Tottenham Hotspur hadi Juni 8 na mechi yao ya pili ya kujipima nguvu itakuwa dhidi ya Austria mjini Vienna Juni 10.
  Mabingwa hao mara tano wa Kombe la Dunia, Brazil wapo Kundi E na watafungua dimba na Uswisi mjini Rostov-on-Don Juni 17, kabla ya kuwavaa Costa Rica mjini Saint-Petersburg na kukamilisha mechi zao za Raundi ya kwanza kuwa kumenyana na Serbia mjini Moscow.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NEYMAR ASEMA BADO HAJISIKII VIZURI SANA, LAKINI ATACHEZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top