• HABARI MPYA

  Monday, May 07, 2018

  NINJE AMCHUKUA KIPA WA ZANZIBAR KUZIBA PENGO LA KABWILI NGORONGORO HEROES

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, Ammy Conrad Ninje amemchukua kipa Peter Doto Mashauri wa Black Sailor ya Zanzibar kuziba pengo la Ramadhan Kabwili wa Yanga SC.
  Ninje amemuengua kikosini moja kwa moja kipa namba moja wa timu hiyo, Kabwili baa ya kukasirishwa na kitendo cha mlinda mlango huyo kuondoka na klabu yake, Yanga kwenda Algeria.
  Ninje alitaka Kabwili arejee kwenye kwenye kambi ya Ngorongoro baada ya kuruhusiwa kwenda kuichezea Yanga katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikifungwa 1-0 na mahasimu, Simba SC Aprili 29, uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ramadhan Kabwili ametemwa moja kwa moja Ngorongoro Heroes kwa sababu ya Yanga

  Lakini kipa huyo wa pili wa Yanga kwa sasa, akaunganisha na timu yake kwa safari ya Algeria ambako jana ilicheza na kufungwa 4-0 na wenyeji, USM Alger katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika.
  Ninje akasema kitendo cha Kabwili kuunganisha safari na Yanga Algeria ni cha utovu wa nidhamu na hamhitaji tena atateua mchezaji mwingine kuziba nafasi yake, ambaye ndiye huyu Peter Doto Mashauri.  
  Ngorongoro ipo kambini Mbweni, Dar es Salaam ikijiandaa na mchezo wa Raundi ya Pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa 20 mwakani nchini Niger dhidi ya Mali Jumapili Uwanja wa Taifa. 
  Hiyo ni baada ya kuitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Raundi ya Kwanza kwa penalti 6-5 mjini Kinshasa baada ya sare mbili za 0-0 nyumbani na ugenini, mechi zote Kabwili akidaka kwa ustadi mkubwa kuanzia Dar es Salaam kabla ya kwenda kuokoa penalti kwenye mechi ya marudiano na kuivusha Ngorongoro hadi hatua hii.     
  Kabwili alikuwa namba moja wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za U17 za Afrika nchini Gabon Mei mwaka jana, ambayo wachezaji wake wengi ndiyo wanaunda Ngorongoro kwa sasa na wazi kuondolewa kwake ni pigo kwa timu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NINJE AMCHUKUA KIPA WA ZANZIBAR KUZIBA PENGO LA KABWILI NGORONGORO HEROES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top