• HABARI MPYA

  Sunday, May 27, 2018

  YANGA SC YARUDISHA NYUMA MKUTANO WAKE KWA WIKI MOJA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MKUTANO Mkuu wa mwaka wa klabu ya Yanga SC uliokuwa umepangwa kufanyika Jumamosi Juni 17, mwaka huu umerudishwa nyuma kwa wiki moja hadi Juni 10 na utafanyika mjini Dar es Salaam katika ukumbi ambao utatajwa baadaye.
  Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika jana mjini Dar es Salaam na katika mkutano huo wanachama wa kadi zote wataruhusiwa kuingia – tu wawe wamezilipia.
  “Kadi za uanachama mpya za Posta na za zamani zote zitatumika. Jambo la kuzingatia ni kwamba lazima ziwe hai zimelipiwa ada na mwanachama lazima awepo katika kitabu ch orodha ya wanachama wa klabu na tawi lake,”amesema Mkwasa. 

  Ikumbukwe Yanga imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji Mei mwaka jana.
  Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
  Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
  Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
  Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
  Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
  Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
  Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
  Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
  Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
  Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
  Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
  Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YARUDISHA NYUMA MKUTANO WAKE KWA WIKI MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top