• HABARI MPYA

  Friday, May 25, 2018

  TSHISHIMBI, AJIBU WAREJEA YANGA IKIIVAA RUVU SHOOTING LEO UWANJA WA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  VIGOGO wa soka nchini, Yanga SC leo wanateremka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Yanga SC wanahitaji kushinda mchezo wa leo katika harakati zake za kusaka heshima ya kumaliza nafasi ya pili kufuatia kuvuliwa ubingwa wa Ligi Kuu na mahasimu wao wa jadi, Simba SC.
  Kwa Ruvu Shooting mchezo wa leo ni wa heshima na kudhihirisha ubora wao kama timu ni ubora wa wachezaji wake mmoja mmoja.
  Kwa sababu hiyo mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu leo kutokana na kila timu kuingia uwanjani kwa dhamira ya kusaka ushindi.

  Papy Kabamba Tshishimbi (kushoto) amerejea kutoka kwao DRC akiwa na anatarajiwa kuanza leo

  Wachezaji wa Yanga leo wanatarajiwa kuingia kwa ari baada ya kulipwa malimbikizo ya mishahara yao ya miezi miwili iliyopita.
  Na habari njema zaidi ni kwamba, kiungo Papy Kabamba Tshishimbi aliyekuwa kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa matibabu amerejea akiwa fiti na amefanya mazoezi na wenzake kwa siku tatu ziliziopita kuelekea mchezo wa leo.
  Naye kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu Migomba aliyekuwa anauguliwa na mwanawe amejiunga na wenzake kwa siku tatu zilizopita na amekuwa mazoezini pia kuashiria yuko fiti na anaweza kucheza.
  Kipa wa pili, Ramadhani Awam Kabwili na winga chipukizi Said Mussa waliokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes nao wamerejea jana na haitakuwa ajabu wakijumuishwa kwenye orodha ya wachezaji wa kushiriki mechi ya leo.     
  Kwa ujumla leo inatarajiwa Yanga iliyo imara kidogo baada ya muda wa takriban mwezi mmoja, jambo ambalo linawapa matumaini ya ushindi wapenzi wa timu hiyo.  
  Ikumbukwe ni Jumanne tu Yanga ilifuta mkosi, baada ya kushinda mechi ya kwanza tangu ikimbiwe na aliyekuwa kocha wake, Mzambia George Lwandamina kufuatia kuilaza 1-0 Mbao FC Uwanja wa Taifa, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 26.
  Ushindi huo uliifanya Yanga SC ifikishe pointi 51 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 55 za mechi 29 na mabingwa tayari, Simba SC wenye pointi 68 za mechi 29.
  Baada ya mechi na Ruvu Shooting leo, Yanga SC itamenyana na Azam FC katika mchezo wa mwisho wa msimu Jumatatu Uwanja wa Taifa pia ambao watatakiwa kushindi kama watashinda na leo ili kumaliza nafasi ya pili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TSHISHIMBI, AJIBU WAREJEA YANGA IKIIVAA RUVU SHOOTING LEO UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top