• HABARI MPYA

    Monday, July 11, 2016

    NI URENO BINGWA EURO 2016, UFARANSA AFA 1-0 NYUMBANI

    BAO pekee la Ederzito ‘Eder’ Antonio Macedo Lopes dakika ya 109, limetosha kuipa Ureno ubingwa wa kombe la Mataifa ya Ulaya, maarufu kama Euro 2016 baada ya kuwafunga wenyeji Ufaransa 1-0 Uwanja wa Stade de France mjini Paris.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mark Clattenburg wa England, Eder aliyezaliwa mjini Bissau, Guinea-Bissau, Desemba 22, mwaka 1987 kabla ya kuhamia Ureno alipotimiza miaka 11 alifunga kwa shuti la umbali wa mita 25 baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Renato Sanches dakika ya 79.
    Haukuwa ushindi mwepesi kwa Ureno, kwani ilimpoteza Nahodha wake Cristiano Ronaldo aliyeumia dakika ya 25 na nafasi yake kuchukuliwa na mkongwe Ricardo Quaresma.
    Ronaldo akarejea kwenye benchi kuwasaidia makocha wake kuwaongoza wachezaji wenzake hadi kufanikiwa kutwaa taji hilo. 

    Nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo akiwa ameshika Kombe la Euro 2016 baada ya kukabidhiwa usiku huu PICHA ZAIDI GONGA HAPA 

    Na kwa ushindi huo, Ureno wanapata Euro Milioni 8, wakati Ufaransa wanapata Milioni 5, huku Ujerumani na Wales wote wakipata Milioni 4 kila timu kwa kuishia Nusu Fainali.

    Timu zilizotolewa katika Robo Fainali zitapata Euro Milioni 2.5, wakati zilizoishia 16 Bora zitapata Milioni 1.5 na zilizopata ushindi katika hatua ya makundi zinapata Milioni wakati kwa kufuzu tu kila timu inapata Euro 500,000
    Hii ni mara ya kwanza kwa Ureno kutwaa taji hilo, baada ya awali kukomea Nusu Fainali mara tatu katika miaka ya 1984, 2000 na 2012, wakati Ufaransa ilikuwa inajaribu kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu baada ya mwaka 1984 na 2000.  
    Ureno ilianza Euro 2016 kwa kusuasua baada ya kumaliza mechi za Kundi F bila ushindi ikitoa sare zote, 1-1 na Iceland, 0-0 na Austria na 3-3 na Hungary hivyo kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Hungary na Iceland na kufuzu hatua ya 16 Bora kama mshindi wa tatu bora wa makundi yote. 
    Katika hatua ya 16 Bora ikashinda 1-0 baada ya dakika 120, bao pekee la mkongwe Ricardo Quaresma dakika ya 117 na kwenye Robo Fainali ikashinda kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
    Ureno ikaustaajabisha ulimwengu baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Wales ya Gareth Bale katika Nusu Fainali, mabao ya Nahodha Cristiano Ronaldo dakika ya 50 na Luis Nani dakika ya 53 – kabla ya leo Eder kupeleka taji la Euro 2016 Ureno.
    Ufaransa inapoteza mechi ya kwanza katika mashindano haya, baada ya awali kushinda mechi za Kundi A dhidi ya Romania 2-1 na Albania 2-0 kabla ya kulazimishwa sare ya 0-0 na Uswisi.
    Katika hatua ya 16 Bora iliwatoa Jamhuri ya Ireland kwa kuwafunga 2-1, mabao yake yote yakifungwa na Antoine Griezmann huku la wapinzani wao likifungwa na Brady kwa penalti.
    Katika Robo Fainali iliwatoa Iceland kwa kuwachapa 5-2, mabao yao yakifungwa na Giroud mawili, Paul Pogba, Payet na Griezmann huku ya wapinzani yakifungwa na Sigporsson na B. Bjarnason.
    Na katika Nusu Fainali waliwafunga Ujerumani 2-0, mabao yote akifunga mfungaji bora wa fainali za mwaka huu, Griezmann aliyemaliza na mabao sita ambaye leo alifichwa na mabeki wa Ureno.
    Kikosi cha Ureno kilikuwa; Rui Patricio, Cedric, Pepe, Fonte, Guerreiro, William Carvalho, Renato Sanches/Eder dk79, Adrien Silva/Joao Moutinho dk66, Joao Mario, Nani na Ronaldo/Quaresma. 
    Ufaransa: Lloris, Sagna, Koscielny, Umtiti, Evra, Sissoko/A. Martial dk 110, Pogba, Matuidi, Payet/K. Coman dk58, Griezmann, Giroud/A. Gignac dk78.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI URENO BINGWA EURO 2016, UFARANSA AFA 1-0 NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top