• HABARI MPYA

    Thursday, July 07, 2016

    JERRY MURO AFUNGIWA MWAKA MMOJA NA FAINI MILIONI 3

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3.
    Jerry amefungiwa leo baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es Salaam.
    Na amefungiwa baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF mbele ya Kamati ya Ogunde.
    Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo.
    Jerry Muro amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3

    Kwa kosa hilo akahukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja- wakati shitaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
    Katika shitaka hilo, Jerry anadaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    “Alihamasisha mashabiki wa Yanga kufanya vurugu katika mechi dhidi ya Maembe kwa kusema mashabiki wa Simba hawana haki ya kuingia uwanjani, kwa sababu Uwanja umekodiwa na Yanga. Na hili Kamati ilijiridhisha baada ya kusikiliza sauti zake alipokuwa akihojiwa na vituo vya Redio,”kimesema chanzo jioni hii kutoka kwenye Kamati hiyo.
    Kwa kosa hilo Jerry Muro amefungiwa mwaka mmoja pia na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3 ingawa adhabu zote zinakwenda sambamba – maana yake atakuwa pembeni na masuala ya soka kwa mwaka mmoja tu.
    Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shitaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya Televisheni.
    “Kamati ilisikiliza kwa makini taarifa zake alipokuwa anazungumza na vituo vya Redio na kugundua alikuwa sahihi, hivyo hapa hana hatia,”kimesema chanzo.
    Hata hivyo, Jerry Muro amehukumiwa wakati mwenyewe hakuwepo kwenye kikao na inadaiwa hakutoa taarifa ya maandishi juu ya kutohudhuria kwake.
    Badala yake, imeelezwa Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alifika mapema leo kabla ya kikao kwa ajili ya kutoa taarifa ya mdomo kwamba Muro amekwenda kwao Kilimanjaro kusafisha makaburi ya wazee wake. 
    Lakini Kamati ikaamua kuendelea na kikao kwa mujibu wa kanuni na hatimaye kuchukua hatua ilizochukua. Hata hivyo, Muro ana haki ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JERRY MURO AFUNGIWA MWAKA MMOJA NA FAINI MILIONI 3 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top