• HABARI MPYA

  Tuesday, May 08, 2018

  WAZIRI MWAKYEMBE AIAGIZA BMT YA TENGA KUZUIA UBINAFSISHAJI WA KLABU ZA WANACHAMA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison George Mwakyembe ameutaka uongozi mpya wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha vyama na klabu hawabinafsishi vyama na klabu wanazoziongoza na hivyo kuwavunja mioyo wanachama wao. 
  Waziri Mwakyembe ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi baraza la 14 la michezo la Taifa leo mjini Dar es Salaam, sherehe ambazo zilihudhuriwa na viongozi wapya wa BMT, akiwemo Mwenyekiti, Leodegar Chilla Tenga, Waziri Mwakyembe amesema Serikali imewateua kwa kuzingatia umakini na uwezo wa kila mmoja wakiwa na malengo ya kuongeza ufanisi wa chombo hicho muhimu katika usimamizi wa Maendeleo ya Michezo nchini. 
  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. HarrisonMwakyembe (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa BMT, Leodegar (katikati). Kulia ni Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo

  “Mmeteuliwa ili kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Maendeleo ya Michezo. Kazi kubwa mnayokwenda kuifanya imefafanuliwa vyema katika Sheria inayounda Baraza la Michezo la Taifa, ambayo ni Sheria ya Bunge Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake Namba 6 ya mwaka 1971,”amesema na kuongeza kwamba sheria hiyo imeaainisha vema kazi na wajibu wa BMT katika kuendeleza michezo nchini.
  “Baraza hili litapewa majukumu ya ziada au ya nyongeza kutokana na hali halisi ya michezo ilivyo kwa sasa hapa nchini. Nyongeza hii, itatokana na ukongwe wa Sheria yenyewe, hali inayosababisha baadhi ya kazi kushindwa kutekelezeka kama inavyotarajiwa hivyo yanahitajika maelekezo ya ziada,”amesema.
  Amezitaja kazi za nyongeza ambazo zinahitaji utekelezaji wa haraka ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo nchini ambao utakuwa na vyanzo endelevu vya mapato na Mwakyembe amesema ili kufanikisha jambo hilo, lazima vyanzo vya mapato vya kisheria viboreshwe na vyanzo vipya vibuniwe na kuanzishwa ili kumudu majukumu mapana ya BMT. 
  “Kwa mfano, moja ya chanzo cha mapato ya BMT ni asilimia kumi (10%) ya bei ya kiingilio ya tiketi katika michezo yenye viingilio. Hili halijawahi kutekelezwa na Baraza. Vilevile, ukusanywaji wa maduhuli kutoka katika Michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa haufuatiliwi,”.
  Mambo mengibe aliyioyataja Waziri huyo makini ni; “2. Kuendelea kufanya Mapitio ya Sheria iliyounda BARAZA ili kuwa na Sheria inayoendana na hali halisi pamoja na matakwa ya Maendeleo ya Michezo ya leo Tanzania na Duniani kote,”.
  “3. Chini ya Uongozi wako pamoja na timu uliyonayo hakikisheni mnafanya Mikutano na Wadau wa Michezo katika ngazi za Mikoa na Wilaya kubaini changamoto zao na kufuatilia maendeleo yao. Hivi sasa Mikoa na Halmashauri zote zimejitahidi kuajiri Maafisa Michezo, ambapo kazi yao ni kusimamia na kuhamasisha michezo katika ngazi hizo za Mikoa na Wilaya,”. 
  “Iwapo kutakuwa na mipango endelevu ya Maendeleo ya Michezo katika ngazi ya Taifa (BARAZA) hadi Wilaya ambako ndiko chimbuko la vipaji vya michezo na mipango hiyo ikisimamiwa vilivyo kwa ushirikiano baina ya BMT, Mikoa na Wilaya, ni dhahiri tutapata maendeleo mazuri katika Sekta ya Michezo. Ili kufanikiwa katika jambo hili, ninaliagiza Baraza lako kuhakikisha kuwa linaongeza ushirikiano kwa kupitia Vikao na Mikutano yenye tija kwa Mikoa na Wilaya zote,”.
  “4. Kutoa mafunzo ya Utawala bora na namna nzuri ya kuongoza Vyama na Mashirikisho ya Kitaifa ili kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro isiyo ya lazima na kuleta ustawi katika kuendeleza michezo nchini,”.
  “5. Nina matarajio makubwa chini ya uongozi wako, kwamba kwa mara ya kwanza BARAZA litatekeleza matakwa ya Sheria ya kuandaa tarifa kila mwaka za utendaji na shughuli za BARAZA ambazo, kwa mujibu wa Sheria, zikiwasilishwa kwangu, na mimi naziwasilisha Bungeni,”.
  “6. BARAZA lihakikishe kuwa vyama vya michezo vinaheshimu Katiba zao kwa kuheshimu VIPINDI VYA UONGOZI na KUFANYA UCHAGUZI muda unapofika. Tuhakikishe kuwa viongozi hawabinafsishi vyama wanavyoviongoza na hivyo kuwavunja moyo wanachama wao. Natuhakikishe kuwa viongozi wa vyama vya michezo (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Waweka Hazina hawashiki nafas iza uongozi zaidi ya MOJA kwenye vyama tofauti katika aina moja ya mchezo,”.
  Mwakyembe amesema anaweza kuendelea kuagiza utekelezwaji wa kazi nyingine nyingi, lakini anaamini hizi chache pamoja na zile zilizopo katika Sheria ya BMT zikitekelezwa vizuri, Maendeleo ya Michezo hayawezi kuwa ndoto ya mbali sana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAZIRI MWAKYEMBE AIAGIZA BMT YA TENGA KUZUIA UBINAFSISHAJI WA KLABU ZA WANACHAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top