• HABARI MPYA

  Tuesday, May 08, 2018

  KOCHA MPYA MKONGO ASHAURI YANGA B IMALIZIE LIGI KUU, KIKOSI CHA KWANZA KIKOMAE LA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA mpya mtarajiwa wa Yanga SC, Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ameshauri uongozi kupeleka kikosi cha timu ya vijana, maarufu kama Yanga B katika mechi zake mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhid ya Tanzania Prisons mjini Mbeya na Mtibwa Sugar mjini Morogoro, ili kikosi cha kwanza kiendelee na maandalizi ya mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Jumatano ijayo.
  Zahera amesema kwa sasa Yanga wanapaswa kuelekeza nguvu zao kwenye mechi za Kombe la Shirikisho la Soka Afrika baada ya kupoteza nafasi ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.
  Zahera ameyasema hayo leo mchana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam wakati kikosi cha Yanga kikiwasili kutoka Algiers nchini Angeria ambako Jumapili kilifungwa mabao 4-0 na wenyeji, U.S.M. Alger katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho Uwanja wa Julai 5, 1962.

  “hatuna nafasi kwenye ligi, hivyo tunatakiwa kuweka nguvu zote kwenye kombe la Shirikisho, nimewaomba viongozi wapeleke kikosi B katika michezo yetu ya ligi, ili nibaki na kikosi cha kwanzaa nikiandae kwa ajii ya mchezo dhidi ya Rayon,”. 
  "Tunatakiwa kujiandaa vema ili tusipoteze mchezo huo, ukiangalia ratiba ya ligi imekaa vibaya kwetu,  tumefika leo, kesho tunatakiwa kwenda Mbeya, baadaye tuna mchezo Morogoro, kabla ya kuivaa Rayon,  ndio maana nimewaomba wakubwa tuwaze zaidi kombe la Shirikisho,”amesema.
  Akizungumzia kipigo cha Algeria, Zahera alisema kikosi chake kiipoteza mchezo huo kutokana na kukosa wachezaji wazoefu; “Tulipoteza mchezo kwa kukosa uzoefu, hatukuwa na wachezaji wetu wazoefu, hivyo uwanjani tulikuwa na watoto watano, wenzetu walitumia mwanya huo kutuadhibu. Kwenye mpira uzoefu ni jambo la msingi, vijana walijitahidi kucheza kwenye majukumu waliyopewa, lakini walikosa umakini,”alisema.
  Yanga SC imepoteza nafasi ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu, kufuatia kufungwa 1-0 na mahasimu wao, Simba SC Aprili 29, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao pekee la Erasto Edward Nyoni na sasa Wekundu wa Msimbazi watahitaji kushinda mechi yao ijayo dhidi ya Singida United Jumapili kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu.  
  Simba ina pointi 65 baada ya kucheza mechi 27 na Yanga yenye pointi 48 za mechi 24, inaweza kumaliza na pointi 66 ikishinda mechi zake zote zilizosalia- maana yake hata wakitoa sare na Tanzania Prisons keshokutwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Wekundu wa Msimbazi watatawazwa kuwa wafalme wa Tanzania Bara.
  Baada ya mechi na Prisons Alhamisi, Yanga watasogea mjini Morogoro kumenyana na Mtibwa Sugar Jumapili, kabla ya Jumatano kuteremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Rayon Sport katika mechi ya Kundi D. 
  Michuano ya Kombe la Shirikisho itasimama baada ya mechi za katikati ya wiki ijayo, Yanga na Rayon na Gor Mahia na USM Alger kupisha Fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi. Yanga watakamilisha mechi zao za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
  Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA MPYA MKONGO ASHAURI YANGA B IMALIZIE LIGI KUU, KIKOSI CHA KWANZA KIKOMAE LA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top