• HABARI MPYA

    Wednesday, May 09, 2018

    RAIS KARIA AMREJESHA KIPA RAMADHANI KABWILI NGORONGORO HERORES

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KIPA wa Yanga SC, Ramadhahi Awam Kabwili amejiunga na kambi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace kumaliza tofauti kati ya kipa huyo na kocha Ammy Conrad Ninje.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF, Karia amesema kwamba Kabwili amekwishajiunga na wenzake kambini kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Mali kufuzu Fainali za Afrika za U20 mwakani nchini Niger.
    “Kilichotokea hadi kabwili kwenda nchini Algeria kuitumikia timu yake ya Yanga kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya U.S.M Alger ni kutokuwa na mawasiliano mazuri kati ya uongozi wa TFF na uongozi wa klabu ya Yanga,”amesema Karia.
    Ramadhahi Kabwili amejiunga na kambi ya Ngorongoro Heroes baada ya Rais wa TF), Wallace kumaliza tofauti kati yake na kocha Ammy Ninje

    Kocha wa Ngorongoro Heroes, Ammy Conrad Ninje aliamua kumchukua kipa Peter Doto Mashauri wa Black Sailor ya Zanzibar kuziba pengo la Ramadhan Kabwili wa Yanga SC baada ya kukasirishwa na kitendo cha mlinda mlango huyo kuondoka na klabu yake, Yanga kwenda Algeria bila ruhusa yake.
    Ninje alitaka Kabwili arejee kwenye kwenye kambi ya Ngorongoro baada ya kuruhusiwa kwenda kuichezea Yanga katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikifungwa 1-0 na mahasimu, Simba SC Aprili 29, uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Lakini kipa huyo wa pili wa Yanga kwa sasa, akaunganisha na timu yake kwa safari ya Algeria ambako Jumapili ilifungwa 4-0 na wenyeji, USM Alger katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika.
    Ninje akasema kitendo cha Kabwili kuunganisha safari na Yanga Algeria ni cha utovu wa nidhamu na hamhitaji tena atateua mchezaji mwingine kuziba nafasi yake, ambaye ndiye huyu Peter Doto Mashauri.  
    Ngorongoro ipo kambini Mbweni, Dar es Salaam ikijiandaa na mchezo wa Raundi ya Pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa 20 mwakani nchini Niger dhidi ya Mali Jumapili Uwanja wa Taifa. 
    Hiyo ni baada ya kuitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Raundi ya Kwanza kwa penalti 6-5 mjini Kinshasa baada ya sare mbili za 0-0 nyumbani na ugenini, mechi zote Kabwili akidaka kwa ustadi mkubwa kuanzia Dar es Salaam kabla ya kwenda kuokoa penalti kwenye mechi ya marudiano na kuivusha Ngorongoro hadi hatua hii.     
    Kabwili alikuwa namba moja wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za U17 za Afrika nchini Gabon Mei mwaka jana, ambayo wachezaji wake wengi ndiyo wanaunda Ngorongoro.
    Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limewateua marefa kutoka Comoro kuchezesha mechi hiyo, ambao ni Soulaimane Ansudane atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera Mmadi Faissoil na Abdoulmadjid Azilani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS KARIA AMREJESHA KIPA RAMADHANI KABWILI NGORONGORO HERORES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top