• HABARI MPYA

  Monday, May 07, 2018

  KOCHA WA ZAMANI WA YANGA, JACK CHAMANGWANA AFARIKI DUNIA MALAWI AKIWA ANA UMRI WA MIAKA 61

  Na Mwandishi Wetu, BLANTYRE
  KOCHA wa zamani wa klabu ya Yanga SC, Jack Lloyd ‘Africa’ Chamangwana amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Queen Elizabeth Central (QECH) mjini Blantyre akiwa ana umri wa miaka 61.
  Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi amefariki akiwa shujaa wa taifa lake na gwiji wa soka ya nchi yake pia mwenye heshima kubwa.
  Hadi anakutwa na umauti, Chamangwana alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Be Forward Wanderers na alikuwa kocha mkuu wa Nomads hapo kabla.
  Baada ya kuichezea The Flames mechi 133 akiwa na Nahodha pia na kuwemo kwenye kikosi kilichobeba Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka 1978- 1979, Chamangwana akawa Kocha wa Malawi na Mkurugenzi wa Ufundi.
  Jack Chamangwana (kushoto) amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Queen Elizabeth Central (mjini Blantyre 

  Mara ya mwisho alikuwa Kocha Msaidizi wa timu hiyo chini ya Young Chimodzi hadi Juni 2015 walipoondolewa na Chama cha Soka Malawi (FAM). 
  Alikuwemo kwenye kikosi cha kwanza kabisa cha Malawi kilichocheza fainali zake za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ivory Coast mwaka 1984 na akawa katika benchi la Ufundi wakati timu hiyo ikishiriki AFCON ya mwaka 2010 nchini Angola kama Mkuruhenzi wa Ufundi chini ya kocha, Kinnah Phiri.
  Jack ‘Africa’ Chamangwana alistaafu soka mwaka 1985 baada ya kucheza hadi Afrika Kusini katika klabu ya Kaizer Chiefs na mwaka 2002 alikuja Tanzania kuifundisha klabu ya Yanga kwa wakati tofauti, akiingia na kutoka hadi mwaka 2006 alipohamia Maji Maji ya Songea kabla ya kurejea kwao Malawi. Mungu ampumzishe kwa amani Chamangwana. Amin.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA WA ZAMANI WA YANGA, JACK CHAMANGWANA AFARIKI DUNIA MALAWI AKIWA ANA UMRI WA MIAKA 61 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top