TIMU ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC leo yamefungwa na winga mpya wa kushoto, Libasse Gueye (22) aliyesajiliwa mwezi huu katika dirisha dogo kutoka Teungueth FC ya kwao, Senegal dakika ya 27 na mshambuliaji Suleiman Abdallah Mwalimu 'Gomez' anayecheza kwa mkopo tangu mwanzo wa msimu kutoka Wydad Athletics dakika ya 76.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 16 katika mchezo wa saba na kusogea nafasi ya nne, wakati Mashujaa FC inabaki na pointi zake 13 za mechi 11 sasa nafasi ya nane.
Baada ya mchezo huo, Simba SC inarejea kambini kujiandaa na mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Espérance ya Tunisia Jumapili kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ili kufufua matumaini ya kwenda Robo Fainali, Simba inahitaji kushinda Jumapili ikitoka kufungwa mechi zote tatu za mwanzio ikiwemo ya Jumamosi ambayo walifungwa 1-0 na Espérance Uwanja wa Hammadi Agrebi Jijini Tunis nchini Tunisia.
Bao lililoizamisha Simba SC siku hiyo lilifungwa na winga chipukizi wa umri wa miaka 19 wa Burkina Faso, Jack Diarra dakika ya 21 akimtungua kipa wa Kimataifa wa Niger, Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo.



.png)
0 comments:
Post a Comment