MABINGWA watetezi, Young Africans, maarufu tu kama Yanga SC wametoka nyuma na kushinda mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao Yanga SC yamefungwa na washambuliaji wake wa kigeni, Muangola Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ mawili kwa penalti dakika ya 45’+2 na la kichwa dakika ya 60 na Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo dakika ya baada ya 66,
Na hiyo ilikuwa baada ya mshambuliaji mzawa, William Edgar kuanza kuifungia Dodoma Jiji FC dakika ya 41 akiwatoka kwa ustadi mkubwa mabeki wa Yanga kabla ya kumtungua kipa namba moja wa Mali, Djigui Diarra.
Kwa ushindi huo, Yanga SC wanafikisha pointi 22 katika mchezo wa nane na kurejea kileleni ikiishushia nafasi ya pili JKT Tanzania yenye pointi 21 za mechi 12.
Kwa upande wao Dodoma Jiji baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi 10 za mechi 10 nafasi ya 11.
Baada ya mchezo huo Yanga wanakwenda Zanzibar kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri Jumamosi ya Januari 31 Uwanja wa New Amaan Complex.
Ikumbukwe Yanga ilichapwa 2-0 na wenyeji, Al Ahly Ijumaa ya Januari 23 mabao ya winga wa kushoto, Mahmoud Ahmed Ibrahim Hassan ‘Trézéguet’ moja kila kipindi, dakika ya 45’+3 na 75 Ijumaa usiku huu Uwanja wa Borg El Arab Jijini Alexandria, Misri.



.png)
0 comments:
Post a Comment