MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa tayari wamekwishapata mabao matatu yakifungwa na viungo, Mguinea aliyechukua uraia wa Tanzania, Mohamed Damaro Camara dakika ya nane, Mkenya Duke Ooga Abuya dakika ya 28 naa Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua dakika ya 33.
Kipindi cha pili mshambuliaji Mzimbabwe Prince Dube Mpumelelo alifunga la nne dakika ya 79, kabla ya kiungo mzawa, Mudathir Yahya Abbas kufunga la tano dakika ya 81 na mshambuliaji mpya, Muangola Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ akakamilisha shangwe za mabao dakika ya 89.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 19 katika mchezo wa saba na kurejea kileleni ikiizidi pointi mbili JKT Tanzania ambayo pia imecheza mechi tatu zaidi.
Kwa upande wao Mashujaa baada ya kupoteza huo wanabaki na pointi zao 13 za mechi 10 sasa katika nafasi ya tano.
Baada ya mchezo huo, Yanga SC inatarajiwa kuondoka nchini Alfajir ya keshokutwa kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Al Ahly Ijumaa kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo.




.png)
0 comments:
Post a Comment