VIGOGO wa soka wa Hispania, Real Madrid wametangaza kwamba meneja wao, Xabi Alonso, ameondoka klabuni kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya michezo 28 pekee.
Kiungo huyo wa zamani wa Liverpool aliteuliwa mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuondoka Bayer Leverkusen, ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa Ujerumani mwaka 2024.
Nafasi yake imechukuliwa na mchezaji mwingine wa zamani wa Liverpool, Alvaro Arbeloa, ambaye amekuwa kocha wa timu B ya Real Madrid tangu Juni mwaka jana na pia alitumia miaka sita iliyopita akifanya kazi na akademi.
Alonso anaondoka Real ikiwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa La Liga, ikizidiwa pointi nne na wapinzani wao, Barcelona katikati ya msimu.
Alipata asilimia bora ya ushindi kuliko kocha mkuu yeyote wa Real Madrid katika muongo mmoja uliopita.
Lakini klabu hiyo ilifungwa mabao 3-2 na vinara wa La Liga, Barcelona, katika mchezo wa Fainali ya Super Cup ya Hispania Jumapili ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo wanapoteza.
Kikosi cha Alonso pia kimepoteza kwa Liverpool na Manchester City katika Ligi ya Mabingwa msimu huu. Real ilimaliza ya pili katika LaLiga msimu uliopita.
Real Madrid ilisema klabu hiyo iliachana na Alonso kwa "makubaliano ya pande zote".
"Xabi Alonso atakuwa na mapenzi na pongezi kutoka kwa mashabiki wote wa Madrid kwa sababu yeye ni gwiji wa Real Madrid na amekuwa akiwakilisha maadili ya klabu yetu," taarifa ilisema. "Real Madrid itakuwa nyumbani kwake kila wakati."
Alonso hapo awali alihusishwa na kuhamia Liverpool wakati Jurgen Klopp alipotangaza kwamba angeondoka Anfield mwaka 2024 - lakini akachagua kubaki Leverkusen kwa msimu mwingine kabla ya kuhamia Madrid.
Alisaini mkataba wa miaka mitatu mwezi Mei kumrithi Mtaliano Carlo Ancelotti, ambaye aliondoka klabuni hapo na kuwa kocha mkuu wa Brazil.
Alijijengea heshima kubwa baada ya kuifunga Barcelona 2-1 Uwanja wa Bernabeu Oktoba mwaka jana na kukataa uteja wa kufungwa mechi sita mfululizo na mahasimu wao hao, lakini Real ilishinda mechi mbili tu kati ya nane zilizofuata katika mashindano yote.



.png)
0 comments:
Post a Comment