TIMU ya Azam FC imetoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Nairobi United katika mchezo wa Kundi B Kombe la Shirikisho Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa wa Nyayo Jijini Nairobi.
Mshambuliaji Duncan Oluoch alianza kuifungia Nairobi United dakika ya 14, kabla ya mshambuliaji Mkongo, Jephte Kitambala Bola kuisawazishia Azam FC dakika ya 17 na kipa Mghana, Ernest Mohammed akajifunga dakika ya 78 akijaribu kuokoa kuipatia timu ya Tanzania bao la ushindi.
Azam FC inapata ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, ikifungwa 2-0 na wenyeji Maniema United huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na 1-0 dhidi ya Wydad Athletics Club ya Morocco visiwani Zanzibar.
Kwa Upande wao Nairobi United wanapoteza mechi ya tatu mfululizo ya Kundi B kufuatia kufungwa 3-0 na Wydad AC Jijini Casablanca na 1-0 nyumbani dhidi ya Maniema United.
Mchezo mwingine wa Kundi B utafuatia Saa 2:00 usiku baina ya Wydad AC na AS Maniema Union Uwanja wa Mohammed V Jijini Casablanca kabla ya timu hizo kurudiana Februari 1 Uwanja wa Martyrs Jijini Kinshasa.
Azam FC inarejea nyumbani kujipanga kwa mchezo wa marudiano na Nairobi United Februari 1 pia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.



.png)
0 comments:
Post a Comment