• HABARI MPYA

    Friday, May 11, 2018

    YONDAN ‘AKACHA’ KIKAO CHA KUMJADILI KWA KUMTEMEA MATE ASANTE KWASI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa Yanga SC, Kevin Patrick Yondan juzi hakutokea katika kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kwa ajili ya kesi yake ya kumtemea mate mchezaji wa Simba SC, Mgaha  Asante Kwasi Aprili 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Kutokana na Yondan kutotokea, Kamati imeagiza apewe wito wa mwisho ambao kama hatafika kamati itasikiliza shauri lake katika upande mmoja na kulitolea maamuzi.
    Agizo hilo linawahusu pia George Rast na Shaibu Salim wa AFC, kocha Mromania Aristica Cioaba wa Azam FC, meneja wa JKT Mlale, Issa Ngwasho, Hosea John, Rashid Ally, Hamisi Athumani, Casmir Focus wa JKT Msange, Joseph Mkota wa JKT Oljoro, Katregea Kalegea wa Mashujaa FC na Afisa Habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet ambao hawakufika pia biula taarifa.
    Kevin Yondan (katikati) hakutokea katika kesi yake ya kumtemea mate Asante Kwasi  

    Pamoja na hao, agizo hilo linamhusu pia Meneja wa Singida United Ibrahim Mohamed yeye alitoa taarifa ya kufiwa na baba yake mzazi. 
    Katika kikao chake cha juzi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa TFF ilisikilzia mashauri kadhaa ya watu waliohudhuria na kuyatolea maamuzi.
    Shauri la kwanza lilihusu wachezaji wa Villa Squad Nassoro Makoba,Hamza Habibu na Severine Charles ambao katika mchezo uliowakutanisha Villa Squad na Namungo FC walidaiwa kutaka kumpiga Mwamuzi kinyume na kanuni ya 36 ya Ligi Daraja la Pili.
    Kamati baada ya kupitia shauri hilo na kupitia ushahidi uliowasilishwa mbele ya kamati imewakuta na hatia kwa kosa la kutaka kumpiga Mwamuzi kinyume na kanuni ya 36 ya Ligi Daraja la Pili na kutoa adhabu ya kuwafungia mechi tatu na faini ya shilingi laki Tatu kwa kila mmoja,adhabu ambazo zitatumikiwa kwa pamoja kwa mujibu wa kanuni ya 37(12) za ligi Daraja la pili.
    Shauri la pili lililosikilizwa na kamati lilimuhusu Katibu wa Mlandizi Queens Rukia Michael ikihusisha mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Premium Lite kati ya Mlandizi Queens na Kigoma Sisterz ambao anadaiwa kutaka kumpiga Mwamuzi.
    Kamati ilipitia shauri hilo na kumkuta na hatia ya kuvunja kanuni ya 41(2) ya Ligi Kuu ya Wanawake  kwa kosa la kutaka kumpiga Mwamuzi na ameadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hiyo kwa kufungiwa miezi 2 na faini ya shilingi laki 2 adhabu ambazo zinakwenda kwa pamoja.
    Shauri la Tatu lilimuhusu mchezaji wa Transit Camp Hussein Swalehe Nyamandulu ambaye shtaka lake lilikuwa la kutaka kufanya fujo katika benchi la timu ya Toto Africans na kamati imempa onyo kali kwa mujibu wa Ibara ya 10(1) ya kanuni za nidhamu za TFF.
    Shauri la Nne lilimuhusu mchezaji wa Mbeya City Ramadhan Malima ambaye aliingia kushangilia goli la Mbeya City katika mchezo wao dhidi ya Young Africans wakati aakiwa tayari ameoneshwa kadi nyekundu.
    Kamati imemkuta na hatia na amehukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 37(7)(f), amefungiwa mechi 3 na faini ya shilingi Laki Tano lakini kwasababu amekosa mechi moja sasa atatumikia mechi 2 zilizobaki pamoja na onyo kali kwa mujibu wa kanuni ya 10(1) ya kanuni za nidhamu za TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YONDAN ‘AKACHA’ KIKAO CHA KUMJADILI KWA KUMTEMEA MATE ASANTE KWASI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top