• HABARI MPYA

  Monday, May 21, 2018

  WAMBURA ASEMA MUHTASARI WA KUBADILI WATIA SAINI AKAUNTI ZA TFF 'ULIFOJIWA'

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MKURUGENZI wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura amesema kwamba muhtasari wa kubadili watia saini wa akaunti za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ulikuwa wa kughushi.
  Wambura ameyasema hayo leo Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu mjini Dar es Salaam akitoa ushahidi wake katika kesi inayowakabili vigogo watano wa TFF, akiwemo aliyekuwa Rais, Jamal Malinzi na Katibu wake, Celestine Mwesigwa  kuanza kusikilizwa leo.    
  Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wambura alisema yeye ndiye alikuwa muandika muhtasari wa kikao ambacho kinadaiwa kiliazimia kubadili watia saini wa akaunti za TFF, lakini hakukuwa na kitu kama hicho. 
  Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro, Wambura alidai kuwa muhtasari wa Juni 5, mwaka 2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za TFF katika benki ya Stanbic ni wa kughushi na kwamba yeye haufahamu.
  Wambura alidai alikuwepo katika kikao hicho cha Juni 5, mwaka 2016 na hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa benki wa TFF kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.
  Aidha, Wambura mwenye umri wa miaka 49 alisema kwa sasa anapokea mshahara wa Shilingi Milioni 7 kwa mwezi baada ya kuongezwa na uongozi wa sasa wa TFF, chini ya Rais Wallace Karia kutoka Sh. Milioni 2 alizokuwa analipwa wakati wa Malinzi.
  Akiongozwa na wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza kutoa ushahidi wake, Wambura amebainisha kuwa aliwahi kuwasilisha maombi ya kutaka kuongezwa mshahara kutoka Shilingi Milioni 2 hadi 7 wakati wa utawala wa Malinzi.
  Alipoulizwa na wakili Rweyongeza kwamba Malinzi alikataa kumuongeza mshahara, Wambura alidai kuwa si kweli, lakini alipeleka maombi hayo tena wakati wa utawala wa Rais wa sasa wa TFF, Karia ambaye aliidhinisha alipwe Shilingi Milioni 7 tangu Agosti mwaka jana.
  Ushahidi huo wa Wambura unafuatia Meneja wa benki ya Stanbic tawi la Centre Kinondoni mjini Dar es Salaam, Adelhem Msiagi kusema wiki iliyopita kwamba walikubali mabadiliko ya watia saini wa akaunti za TFF baada ya kujiridhisha taratibu zilifuatwa.

  Boniphace Wambura amesema muhtasari wa kubadili watia saini wa akaunti za TFF ulikuwa wa kughushi


  Msiagi alisema  mwaka 2016 watia saini katika akaunti hizo sita za TFF walikuwa wanne, ambao ni Jamal Malinzi, Wallace Karia, Mwesigwa Selestine na Edgar Masoud, kabla ya Septemba 2, mwaka 2016 Nsiande Mwanga kutambulishwa kuwa mtia saini mpya wa TFF akichukua nafasi ya Edgar Masoud aliyeondolewa.

  Alisema TFF iliwasilisha orodha ya Wajumbe 20 waliopitisha mabadiliko ya kubadili mtia saini kutoka Edgar Masoud hadi Nsiande Mwanga katika kikao kilichohudhuriwa na Wajumbe wa Sekretari sita wakiwamo Mwesigwa, Boniface Wambura na Alfred Lucas.
  Shahidi huyo alidai kuwa makubaliano hayo ya bodi yalisainiwa na rais  wa TFF Jamal Malinzi na Katibu Mkuu na Mwesigwa ambaye ndiyo aliyeyakabidhi makubaliano hayo ya bodi kwa Afisa wa benki na Msiagi aliikabidhi Mahakama nyaraka hizo kama kielezo cha ushahidi Katika kesi hiyo.
  Washitakiwa wengine katika kesi hiyo mbali ya Malinzi mwenye umri wa miaka 57, Mwesigwa miaka 46, ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga mwenye umri wa miaka 27, Meneja Ofisi wa TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 na wanakabiliwa na mashitaka 30.
  Katika mashtaka hayo, Malinzi pekee anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha dola za Kimarekani 173,335 na Sh 43,100,000, wakati Mwesigwa anakabiliwa na mashitaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji wa fedha.
  Nsiande anakabiliwa na mashitaka mawili ya utakatishaji wa fedha, Miriam anakabiliwa na mashitaka tisa ya kughushi na Frola anakabiliwa na shitaka moja la kughushi na wote walikana mashitaka hayo.
  Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, wakati Mirima na Flora wapo nje kwa dhamana.
  Baada ya maelezo ya Wambura leo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 28 na 29 itakaposikilizwa mfululizo, kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAMBURA ASEMA MUHTASARI WA KUBADILI WATIA SAINI AKAUNTI ZA TFF 'ULIFOJIWA' Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top