• HABARI MPYA

    Saturday, May 12, 2018

    SHEREHE ZA UBINGWA SIMBA SC NI LEO SINGIDA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itaendelea leo kwa mechi mbili tu, Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Njombe Mji FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Singida United wakiwakaribisha SImba SC Uwanja wa Namfua, Singida.     
    Simba SC wanacheza mechi ya kwanza leo tangu wawe mabingwa rasmi wa Ligi Kuu baada ya waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC kulitema rasmi taji hilo juzi kufuatia kufungwa mabao 2-0 na wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Kwa maana hiyo, pointi 65 ambazo wamejikusanyia Simba SC hadi sasa zinawatosha kuitwa mabingwa, kwani Yanga wenye pointi 48 kwa sasa baada ya kucheza mechi 25, hata wakishinda mechi zao zote zilizosalia watafikisha pointi 63 tu.

    Yanga inauachia ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kukaa nao kwa misimu mitatu mfululizio wakati, Simba SC inatwaa taji la kwanza la ligi hiyo tangu mwaka 2012 walipochukua kwa mara ya mwisho.
    Ikumbukwe usiku wa jana, Azam FC ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea  Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Ushindi huo umetokana na mabao ya mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda dakika ya 49 na kiungo Frank Raymond Domayo dakika ya 57 na Azam FC inafikisha pointi 52, baada ya kucheza mechi 28 nyuma ya mabingwa, Simba SC wenye pointi 65 za mechi 27 na Yanga wenye pointi 48 za mechi 25.
    Maji Maji inazidi kujiweka hatarini kushuka Daraja baada ya kipigo cha leo, kwani inabaki na pointo zake 24 baada ya mechi 29 na ili kubaki Ligi Kuu itabidi iziombee duwa mbaya Ndanda FC yenye pointi 23 za mechi 28 na Njombe Mji FC yenye pointi 22 za mechi 27.
    Timu mbili zitaremka Daraja wiki mbili zijazo na tayari African Lyon, KMC na JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Biashara United ya Mara na Alliance Schools ya Mwanza zimepanda katika Ligi Kuu ya msimu ujao itakayokuwa na timu 20.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHEREHE ZA UBINGWA SIMBA SC NI LEO SINGIDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top