• HABARI MPYA

    Thursday, May 17, 2018

    SHAHIDI KESI YA MALINZI ASEMA; “TULIKUBALI KUBADILI WATIA SAINI TFF BAADA YA KUJIRIDHISHA TARATIBU ZILIFUATWA”

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MENEJA wa benki ya Stanbic tawi la Centre Kinondoni mjini Dar es Salaam, Adelhem Msiagi amesema kwamba walikubali mabadiliko ya watia saini wa akaunti za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kujiridhisha taratibu zilifuatwa.
    Msiagi ameyasema hayo leo Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu mjini Dar es Salaam baada ya kesi inayowakabili vigogo watano wa TFF, akiwemo aliyekuwa Rais, Jamal Malinzi na Katibu wake, Celestine Mwesigwa  kuanza kusikilizwa leo.    
    Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Msiagi aliiambia Mahakama kwamba TFF ni wateja wao kwa sababu wana akaunti sita katika benki yao ambazo watia saini wake ni sita pia. 

    Kesi ya vigogo wa TFF, Jamal Malinzi (kushoto) na Selestine Mwesigwa (kulia) imeanza kusikilizwa leo

    Kimaro alianza kwa kuwakumbusha washitakiwa hao, mashitaka 30 yanayowakabili kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa na ndipo shahidi huyo alisema majukumu yake ni kusimamia shughuli za uendeshaji wa tawi hilo la benki na kutoa huduma kwa wateja ikiwamo kuingiza wateja wapya.
    Alidai wateja wapya kwa Taasisi inapoingia baada ya kukamilisha utaratibu wa kufungua akaunti, inatakiwa kuwasilisha makubaliano ya bodi kwa mujibu wa Katiba yao inayoambatanishwa pia, cheti cha usajili, muhtasari wa kikao ambacho kiliamua na kuteua watia saini na utambulisho wa walioteuliwa.
    “Hayo yakikamilika wanapatiwa fomu kwa ajili ya kufungua akaunti na utaratibu huo ukikamilika wanapokea nyaraka zote wao kama benki zinawekwa kwenye faili na kugongwa muhuri na kutiwa saini na Meneja wa tawi kwa ajili ya kuthibitisha,” alidai Msiagi.
    Alidai kuwa mwenye akaunti ya tasisi akitaka kubadilisha watia saini anapaswa kupeleka benki makubaliano mengine ya bodi yakionyesha kikao kilichoketi na kufikia mabadiliko hayo na kwamba wale wenye dhamana hiyo ndiyo humpeleka yule aliyeteuliwa.
    Alidai Afisa wa benki huyaangalia makubaliano hayo ya bodi kama yapo sawa kabla ya kuyagonga muhuri na kuyapeleka kwa Meneja ili kupata ridhaa na kuyatunza.
    Alidai mwaka 2016 watia saini katika akaunti hizo sita ni walikuwa wane, ambao ni Jamal Malinzi, Wallace Karia, Mwesigwa Selestine na Nsiande Mwanga, kabla ya Septemba 2, mwaka 2016 Nsiande kutambulishwa kuwa mtia saini mpya wa TFF akichukua nafasi ya Edgar Masoud aliyeondolewa.
    Alisema TFF iliwasilisha orodha ya Wajumbe 20 waliopitisha mabadiliko ya kubadili mtia saini kutoka Edgar Masoud hadi Nsiande Mwanga katika kikao kilichohudhuriwa na Wajumbe wa Sekretari sita wakiwamo Mwesigwa, Boniface Wambura na Alfred Lucas.
    Shahidi huyo alidai kuwa makubaliano hayo ya bodi yalisainiwa na rais  wa TFF Jamal Malinzi na Katibu Mkuu na Mwesigwa ambaye ndiyo aliyeyakabidhi makubaliano hayo ya bodi kwa Afisa wa benki na Msiagi aliikabidhi Mahakama nyaraka hizo kama kielezo cha ushahidi Katika kesi hiyo.
    Washitakiwa wengine katika kesi hiyo mbali ya Malinzi mwenye umri wa miaka 57, Mwesigwa miaka 46, ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga mwenye umri wa miaka 27, Meneja Ofisi wa TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 na wanakabiliwa na mashitaka 30.
    Katika mashtaka hayo, Malinzi pekee anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha dola za Kimarekani 173,335 na Sh 43,100,000, wakati Mwesigwa anakabiliwa na mashitaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji wa fedha.
    Nsiande anakabiliwa na mashitaka mawili ya utakatishaji wa fedha, Miriam anakabiliwa na mashitaka tisa ya kughushi na Frola anakabiliwa na shitaka moja la kughushi na wote walikana mashitaka hayo.
    Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, wakati Mirima na Flora wapo nje kwa dhamana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHAHIDI KESI YA MALINZI ASEMA; “TULIKUBALI KUBADILI WATIA SAINI TFF BAADA YA KUJIRIDHISHA TARATIBU ZILIFUATWA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top