• HABARI MPYA

    Thursday, May 17, 2018

    KABWILI AWAFUATA NGORONGORO HEROES LEO KWA MCHEZO WA MARUDIANO NA MALI JUMAPILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIPA Ramadhani Awam Kabwili anaondoka leo Dar es Salaam kuifuata timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Mali Raundi ya pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Vijana chini ya umri wa miaka 20 Afrika mwakani nchini Niger.
    Kabwili hakuwepo kwenye msafara wa Ngorongoro Heroes ulioondoka Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo kwa sababu alikuwa na klabu yake, Yanga SC iliyokuwa inamenyana na Rayon Sport ya Rwanda katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika.
    Na baada ya mchezo huo ambao chipukizi huyo alikuwa benchi akimtazama Mcameroon Youthe Rostand anavyookoa, Kabwili anawafuata wenzake leo kwenda kuipigania bendera ya nchi yake.
    Ramadhani Kabwili anaondoka leo Dar es Salaam kuifuata Ngorongoro Heroes kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Mali Jumapili

    Tanzania ilijiweka kwenye mazingira magumu ya kusonga mbele katika mbio za Niger 2019 baada ya kufungwa mabao 2-1 na Mali kwenye mchezo wa kwanza Mei 13 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Wazi kipigo hicho kilitokana na Kocha Mkuu, Ammy Ninje ambaye kutompanga kipa namba moja, Ramadhani Kabwili ambaye alitofautiana naye kabla ya mchezo wa huo kutokana na kipa huyo kwenda klabu yake, Yanga nchini Algeria kwenye mechi ya ufunguzi ya Kombe la Shirikisho bila kuaga na akamfukuza kwenye timu.  
    Lakini Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alimrejesha kipa huyo kikosini, akisema kilichotokea ni kukosekana kwa mawasiliano mazuri baina ya klabu ya Kabwili na uongozi wa timu na shirikisho.
    Kabwili alikuwa namba moja wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za U17 za Afrika nchini Gabon Mei mwaka jana, ambayo wachezaji wake wengi ndiyo wanaunda Ngorongoro.
    Na ndiye aliyedaka mechi zote mbili Ngorongoro ikiitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Raundi ya Kwanza kwa penalti 6-5 mjini Kinshasa baada ya sare mbili za 0-0 nyumbani na ugenini, kabla ya kwenda kuokoa penalti kwenye mechi ya marudiano na kuivusha Ngorongoro hadi hatua hii.     
    Mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Cameroon na Uganda katika hatua ya mwisho ya mchujo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KABWILI AWAFUATA NGORONGORO HEROES LEO KWA MCHEZO WA MARUDIANO NA MALI JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top