• HABARI MPYA

    Sunday, May 20, 2018

    MKUTANO WA MABADILIKO YA KATIBA SIMBA KUELEKEA KUMKABIDHI TIMU MO WAFANYIKA LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WANACHAMA wa klabu ya Simba SC wanakutana leo katika Mkutano wa mabadiliko ya Katiba utakaofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo eneo la Ocean Road mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 3:00 asubuhi.
    Mkutano huo unakuja siku moja baada ya klabu hiyo kukabidhiwa Kombe ka ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakitoka kufungwa 1-0 na Kagera Sugar. 
    Na inafahamika mkutano huo utakuwa mwepesi, kwa kuwa mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji amekubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu kulingana na maelekezo ya Serikali.

    Mohammed Dewji alikuwepo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Simba ikikabidhiwa Kombe

    Mkutano huo ulioitishwa na Kaimu Mwenyekiti, Salim Abdallah ‘Try Again’ utaanza Saa 3:00 asubuhi na tayari wanachama wamekwishasomewa ajenda kwa mujibu wa Ibara ya 22 ya klabu hiyo, kufungu cha nne.
    Mkutano huo utafuatia ule wa Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji kuwa mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji wa Simba SC.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKUTANO WA MABADILIKO YA KATIBA SIMBA KUELEKEA KUMKABIDHI TIMU MO WAFANYIKA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top