• HABARI MPYA

  Friday, May 11, 2018

  MALIMA WA MBEYA CITY AFUNGIWA MECHI TATU KWA KURUDI UWANJANI MECHI NA YANGA BAADA YA KUTOLEWA KWA KADI NYEKUNDU

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu na kumpiga faini ya Sh. 500,000 beki wa Mbeya City, Ramadhani Malima baada ya kurejea uwanjani kufuatia kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City April 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Akizungumza na Waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF, Msemaji wa shirikisho hilo, Clifford Ndimbo amesema kwamba Kamati ya Saa 72 imepitia mafaili mbalimbali likiwemo la mchezaji wa Mbeya City Malima na kumchukulia hatua dhidi ya kosa alilolifanya katika nchezo huo. 
  Beki wa Mbeya City, Ramadhan Malima (kulia) amefungiwa mechi tatu 

  “Mchezaji Ramadhani Malima alitolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo kati ya Mbeya City na Yanga na baada ya kufungwa kwa bao mchezaji huyo alionekana uwanjani akishangilia na wachezaji wengine. Kutokana na kosa hilo, mchezaji Malima amefungiwa mechi tatu ambayo mechi moja amekwishaitumikia zimebaki mechi mbili na faini ya kiasi cha Sh. 500,000 "amesema Ndimbo.
  Yanga SC ililazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Mbeya City Aprili 22 katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na huo ukawa mwanzo wa kuyeyuka kwa matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa, Shomari Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Omar Juma wa Dodoma na Godfrey Kihwili wa Arusha, Yanga ilitangulia kupata bao lake kipindi chake cha kwanza, kupitia kwa Raphael Daudi Loth kabla ya MCC kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Iddi Suleiman Nado.
  Siku hiyo, Malima alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 65 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kumfuatia kumchezea rafu kiungo wa Yanga, Yussuf Mhilu, lakini akarejea uwanjani kushangilia bao la kusawazisha la timu yake dakika za mwishoni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALIMA WA MBEYA CITY AFUNGIWA MECHI TATU KWA KURUDI UWANJANI MECHI NA YANGA BAADA YA KUTOLEWA KWA KADI NYEKUNDU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top