• HABARI MPYA

    Friday, May 11, 2018

    AZAM FC HAWANA HURUMA NA MAJI MAJI LEO, WANATAKA NAFASI YA PILI

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC leo inateremka Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuvaana na Maji Maji ya Songea mkoani Ruvuma katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku.
    Azam FC leo inaendelea kusaka pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi, hadi sasa ikiwa imejikusanyia pointi 49 katika nafasi ya pili, Yanga yenye mechi tatu mkononi ikiwa nazo 48 huku Simba ikiwa kileleni baada ya kujizolea 65.
    Tayari benchi la ufundi la Azam FC linalosimamiwa na Kocha Msaidizi Idd Cheche na Kocha wa timu ya Azam B, Meja Abdul Mingange, baada ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba kwenda kusoma, limeshawaambia wachezaji juu ya umuhimu wa mechi zilizobakia katika kuhakikisha inashinda zote ili kujiweka pazuri kwenye msimamo.
    Mabingwa hao wa Ligi Kuu msimu wa 2013-2014, Azam FC wataendelea kuwakosa wachezaji wake mabeki Yakubu Mohammed, Swaleh Abdallah, Daniel Amoah, ambao ni majeruhi.
    Wachezaji wengine walioukosa mchezo uliopita kutokana na kuwa wagonjwa, Nahodha Msaidizi Aggrey Morris, kipa Razack Abalora, winga Enock Atta na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, tayari wameanza mazoezi na wenzao kujiandaa na mchezo huo na litabakia ni jukumu la benchi la ufundi kuona kama wanafaa kucheza.
    Wakati Azam FC ikitaka kushinda mchezo huo ili kuendelea kufukuzana na Yanga kuwania nafasi ya pili kwenye msimamo, Majimaji yenyewe itakuwa ikijaribu kusaka pointi ili kuendelea kupambana kutoshuka daraja msimu huu kwani hadi sasa ipo nafasi ya 13 ikiwa imejikusanyia pointi 24 ikiizidi pointi mbili Njombe Mji inayoshika mkia.
    Katika raundi ya kwanza timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea Januari mwaka huu, zilitoka sare ya bao 1-1, Azam FC ikitangulia kufunga kupitia kwa Joseph Mahundi kabla ya Marcel Boniventure kuisawazishia Majimaji kwa mpira wa kona wa moja kwa moja.
    Rekodi mpaka sasa inaonyesha kuwa kihistoria timu hizo zimekutana mara tisa kwenye ligi, Azam FC ikishinda asilimia 98 ya mechi hizo yaani tano, Majimaji ikiwa haijawahi kuonja pointi tatu dhidi ya matajiri hao, huku mechi nne zikiisha kwa sare.
    Mara ya mwisho timu hizo kukutana ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Azam FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa 3-0, mabao mawili yakifungwa na Shomari Kapombe na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, waliohamia Simba msimu huu huku jingine likiwekwa kimiani na kiungo Mudathir Yahya, aliyeenda kwa mkopo Singida United.
    Hadi sasa msimu huu, Azam FC imeshacheza mechi 27 za ligi ikifanikiwa kushinda mara 13, ikitoka sare mechi 10 na kupoteza mara nne, ikiwa imefunga jumla ya mabao 26 na kufungwa 14 ikiwa ni miongoni mwa timu tatu zilizofungwa mabao machache; Simba (13), Azam FC (14), Yanga (14).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC HAWANA HURUMA NA MAJI MAJI LEO, WANATAKA NAFASI YA PILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top