• HABARI MPYA

    Friday, May 11, 2018

    BITEBO AONGEZA NGUVU KAMINI NGORONGORO HEROES, MALI WAWASILI KWA MAFUNGU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMBI ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro imeongezewa nguvu na kijana Abdulrasul Bitebo (pichani kushoto) kutoka akademi ya Aspire nchini Senegal, ambaye aliingia kambini juzi.
    Ngorongoro Heroes watakuwa wenyeji wa Mali, The Eagles Jumapili jioni Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 mwakani Niger.
    Timu hiyo chini ya kocha mwenyeji wa Uingereza mzaliwa wa Dar es Salaam, Ammy Conrad Ninje anayesaidiwa na Juma Mgunda, ipo kambini Mbweni kwa maandalizi ya mchezo huo.
    Mali waliwasili Dar es Salaam jana asubuhi kwa mafungu mawili, la kwanza likiwa na watu tisa na la pili likiwa na watu 20 na wamefikia katika hoteli ya Millennium Tower, Kijitonyama.
    Marefa kutoka Comoro, Soulaimane Ansudane atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera Mmadi Faissoil na Abdoulmadjid Azilani wanatarajiwa kuwasili leo pamoja na Kamisaa kutoka Shelisheli na viingilio katika mchezo huo vitakuwa Sh. 3,000 kwa VIP zote na Sh. 1, 000 kwa mzunguko wote.
    Wakati Ngorongoro hawajawahi kucheza fainali za AFCON U20, mafanikio makubwa ya Mali ni kushika nafasi  ya tatu katika Kombe la Dunia la FIFA la U20 mwaka 1999, baada ya kuifunga Senegal katika mchezo wa kuwania Medali ya Shaba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BITEBO AONGEZA NGUVU KAMINI NGORONGORO HEROES, MALI WAWASILI KWA MAFUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top