• HABARI MPYA

  Thursday, May 17, 2018

  LIPULI FC YAWANYIMA YANGA SC SALAMBA; YAWAAMBIA; “KATAFUTENI MWINGINE, KANUNI ZA CAF HAZIRUHUSU”

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Lipuli FC ya Iringa imekataa ombi la Yanga kumtaka mshambuliaji, Adam Salamba imtumie katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika kwa sababu kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (haziruhusu).
  Barua ya Lipuli kuwajibu Yanga iliyosainiwa na Katibu wa klabu hiyo, Amos Elias Lweramila imesema kwamba hawawezi kumruhusu Salamba kwa sababu kanuni za CAF hata Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na la Tanzania (TFF) haziruhusu.
  “Kanuni za usajili za FIFA, CAF na TFF tumebaini haziruhusu kwa mchezaji Adam Salamba kucheza timu tatu kwa msimu mmoja na zinaruhusu kucheza timu mbili ambazo idadi yake imekoma ambazo ni Stand united na Lipuli,”.
  Katibu huyo, Lweramila amewashauri Yanga kutafuta mchezaji mwingine baada ya mpango wa kumchukua Salamba kugongwa mwamba.
  Lipuli FC imekaata kuwapa Yanga mshambuliaji wao, Adam Salamba kwa sababu kanuni za CAF haziruhusu 

  Pamoja na Salamba, inafahamika Yanga SC pia inamtaka mshambuliaji wa Mbao FC ya Mwanza, Habib Kiyombo na Mnigeria, Quadri Kola anayecheza Botswana.
  Safu ya ushambuliaji ya Yanga ni butu kutokana na kuwakosa wakali wake, Mzimbabwe Donald Ngoma na Mrundi Amissi Tambwe ambao ni majeruhi wa muda mrefu na juhudi za klabu kuongeza wachezaji wapya katika eneo hilo zinaonekana kusuasua. 
  Yanga SC ilipata pointi ya kwanza jana katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika baada ya sare ya bila kufungana na Rayon Sport ya Rwanda katika mchezo wa Kundi D uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa sare hiyo, Yanga inaendelea kushika mkia kwenye kundi hilo, nyuma U.S.M. Alger yenye pointi nne kileleni, Gor Mahia, Rayon pointi mbili kila moja baada ya mechi mbili za awali.
  Ikumbukwe mechi ya kwanza Yanga ilifungwa mabao 4-0 Mei 6 na U.S.M. Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers, Algeria wakati Rayon ililazimishwa sare ya 1-1 na Gor Mahia siku hiyo mjini Kigali.
  Michuano ya Kombe la Shirikisho inasimama sasa kupisha Fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi na Yanga watakamilisha mechi zao za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
  Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
  Timu mbili za juu kutoka kila kundi katika makundi yote manne, zitakutana katika hatua ya Robo Fainali na baadaye Nusu Fainali itakayozaa Fainali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LIPULI FC YAWANYIMA YANGA SC SALAMBA; YAWAAMBIA; “KATAFUTENI MWINGINE, KANUNI ZA CAF HAZIRUHUSU” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top