• HABARI MPYA

  Sunday, May 20, 2018

  KATIBA MPYA YAPETA…RAIS MPYA SIMBA SC NA WAJUMBE WAKE WOTE LAZIMA WAWE NA ‘DEGREE’…

  Na Lisa John, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Simba SC atatakiwa na kiwango cha elimu ya Shahada katika mfumo mpya wa uendeshwaji wa klabu hiyo kwa kuuza hisa.
  Hayo yamefikiwa leo katika mkutano maalum wa kupitisha mabadiliko ya katiba ya Simba SC kuingia kwente mfumo wa soko la hisa, uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam.
  Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama 1,000 na ushei ukiongozwa na Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, marekebisho ya Katiba ya Simba SC yamepita kwa kishindo, wanachama watatu tu wakinyoosha mikono kupinga.
  Kaimu wa Rais wa Simba SC, Salim Abdallah 'Try Again' (kushoto) akimkabidhi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harisson Mwakyembe jezi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli leo mchana wakati wa mkutano wa mabadiliko ya Katiba ya klabu hiyo ukumbi wa Mwalimu Nyerere katikati ya Jiji la Dar es Salaam
  Hapa Kaimu Rais wa Simba, Try Again anamkabidhi Dk. Harrison Mwakyembe jezi iliyosainiwa na wachezaji wa Simba 
  Wanachama wa Simba waliojitokeza mkutanoni leo ukumbi wa Mwalimu Nyerere  

  Katika marekebisho hayo, Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC itakuwa na Wajumbe wanane chini ya Mwenyekiti, ambaye atatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha Shahada sawa na Wajumbe wake watatu wa kuchaguliwa pia.
  Na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
  “Kilichofanyika leo ni historia na demokrasia, kwani wengi wape na ndio walionyoosha mikono, nawaahidi wanachama wenzangu, msimu ujao mtafurahi, kwani tutaanza kutumia Uwanja wetu wa nyumbani, hakuna kitakachoshindikana katika hilo,”alisema Try Again huku akishangiliwa na mamia ya wanachama ukumbini.
  Katika mkutano huo pia, Try Again alimkabidhi Waziri Mwakyembe jezi namba 19, inayobeba idadi ya mataji ya Ligi Kuu ambayo Simba wameshinda ampelekee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli.
  Kwa upande wake, Waziri Mwakyembe amewataka wanachama wa Simba kuepukana na matatizo yatakayoirudisha nyuma klabu yao, kwani dunia nzima kwa sasa klabu zinaendeshwa kwa mfumo wa hisa.
  Kupitishwa kwa mabadiliko ya katiba ndani ya Simba kunafungua milango ya mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji kuwa mwanahisa mkuu wa klabu.
  Hiyo ni baada ya Mo Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
  Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
  Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KATIBA MPYA YAPETA…RAIS MPYA SIMBA SC NA WAJUMBE WAKE WOTE LAZIMA WAWE NA ‘DEGREE’… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top