• HABARI MPYA

  Friday, May 11, 2018

  AZAM FC YAICHIMBIA KABURI MAJI MAJI…YAIPIGA 2-0 CHAMAZI BILA YA HURUMA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Ushindi huo umetokana na mabao ya mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda dakika ya 49 na kiungo Frank Raymond Domayo dakika ya 57 na Azam FC inafikisha pointi 52, baada ya kucheza mechi 28 nyuma ya mabingwa, Simba SC wenye pointi 65 za mechi 27 na Yanga wenye pointi 48 za mechi 25.
  Maji Maji inazidi kujiweka hatarini kushuka Daraja baada ya kipigo cha leo, kwani inabaki na pointo zake 24 baada ya mechi 29 na ili kubaki Ligi Kuu itabidi iziombee duwa mbaya Ndanda FC yenye pointi 23 za mechi 28 na Njombe Mji FC yenye pointi 22 za mechi 27.
  Timu mbili zitaremka Daraja wiki mbili zijazo na tayari African Lyon, KMC na JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Biashara United ya Mara na Alliance Schools ya Mwanza zimepanda katika Ligi Kuu ya msimu ujao itakayokuwa na timu 20.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi mbili tu, Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Njombe Mji FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Singida United wakiwakaribisha SImba SC Uwanja wa Namfua, Singida.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAICHIMBIA KABURI MAJI MAJI…YAIPIGA 2-0 CHAMAZI BILA YA HURUMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top